Ndege iliotoweka yaendelea kutafutwa
29 Desemba 2014Ndege hiyo ya Airbus chapa A320-200 inayomilikiwa na shirika la Air Asia la Indonesia ilitoweka baada ya rubani wake kushindwa kupata ruhusa ya kupaa juu zaidi kutokana na hali mbaya ya hewa, wakati ilipokuwa angani ikitokea mji wa Surabaya nchini Indonesia na kuelekea Singapore siku ya jumapili.
Maafisa wanasema Ndege hiyo yenye nambari ya usajili QZ8501 haikutuma mawasiliano yoyote ya kuwa na matatizo, ilitoweka tu katika eneo la bahari ya Java dakika tano baada ya kuomba kubadili njia ili kukwepa hali mbaya ya hewa, lakini ombi hilo lilikataliwa kutokana na msongamano wa ndege angani.
Hata hivyo timu ya uokozi inaendelea kuitafuta ndege hiyo katika kisiwa cha Belitung mahali ambapo ndege hiyo inaaminika kuanguka. Mkuu wa oparesheni hiyo Joni Superiadi amesema kwa sasa hawajafanikiwa kupata mabaki ya ndege hiyo lakini bado oparesheni zinaendelea.
"Hadi wakati huu bado tunaendelea na shughuli za kuitafuta ndege hiyo iliopoteza mawasiliano, kwa sasa tunaelekea katika kisiwa cha Nangka. Boti nyengine za uokozi pia zinaendelea na shughuli hii ya kutafuta ndege hiyo katika maeneo mengine yalioko karibu, lakini mpaka sasa bado hatujapata mabaki yoyote ya ndege hiyo," alisema Mkuu wa oparesheni hiyo Joni Superiadi.
Raia wengi waliokuwa katika ndege iliotoweka wanatokea Indonesia
Ndege hiyo iliotoweka siku ya Jumapili ilikuwa na abiria 155 kutoka Indonesia, Raia watatu wa Korea Kusini, raia mmoja kutoka Singapore, Mmalasia mmoja na Muingereza mmoja, huku rubani msaidizi wa ndege hiyo akitokea nchini Ufaransa.
Kutoweka kwa ndege hii kunaufanya mwaka huu wa 2014 kuwa mwaka mbaya uliokumbwa na majanga makubwa ya ndege kwa mashirika ya ndege yaliona ushirika na mashirika ya ndege ya Malaysia.
Awali ndege ya Malasia MH370 ilitoweka tarehe 8 mwezi Machi ilipokuwa inatokea Kuala Lumpur kuelekea mjini Beijing, ndege hiyo ilikuwa na abiria 239 pamoja na wafanyakazi wa ndege, mpaka leo haijafanikiwa kupatikana.
Janga jengine lilitokea tarehe 17 mwezi wa Julai ndege ya shirika hilo hilo la Malaysia ilipodunguliwa ikiwa angani nchini Ukraine na kusababisha mauaji ya abiria wote 298 waliokuwa ndani.
Makundi ya ndege za Air Asia wakiwemo washirika wake kutoka Thailand, Ufilipino na India, hawajakuwa na majanga yoyote tangu ndege shirika hilo lilipoanzishwa mwaka wa 2002. Hata hivyo hisa za kundi hilo mjini Kuala Lumpur zimeshuka kwa asilimia nane kuanzia mapema leo asubuhi.
Mwandishi: Amina Abubakar/afp
Mhariri: Iddi Ssessanga