1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ndege yapata ajali

Admin.WagnerD24 Machi 2015

Ndege ya abiria ya shirika la Ujerumani Germanwings imeanguka kusini mwa Ufaransa na watu wote 148 waliokuwamo katika ndege hiyo wanahofiwa kuwa wamekufa.Lakini mpaka sasa sababu ya kutokea ajali hiyo haijajulikana

https://p.dw.com/p/1EwKV
Germanwings 4U9525 Flugzeugabsturz Rettungsaktion in den französischen Alpen
Mahala ambako ndege ya abiria ya Ujerumani iliangukaPicha: picture-alliance/dpa/Photopqr/La Provence/S. Duclet

Ndege hiyo aina ya Airbus, ya shirika tanzu la Lufthansa, Germanwings, ilianguka leo mchana nchini Ufaransa na hakuna matumaini ya kupatikana yeyote alienusurika. Rais wa Ufaransa Francois Hollande amesema mazingira yaliyosababisha ajali, ambayo mpaka sasa bado hayajajulikana yanamfanya mtu aamini kwamba ni vigumu kupatikana mtu yeyote alienusurika katika mkasa huo.

Walikuwamo watu148 katika ndege

Rais Hollande alietoa taarifa juu ya ndege hiyo iliyoangukia nchini mwake amesema hakuna alienusurika kutokana na mazingira yaliyosababisha ajali.

Germanwings Airbus 320
Ndege ya abiria ya Ujerumani iliyoangakaPicha: picture-alliance/dpa/M. Hitij

Maafisa wa Ufaransa wamesema rubani wa ndege alitoa taarifa ya hatari dakika 52 baada ya kuanza safari kutoka mji wa Barcelona nchini Uhispania kuelekea Ujerumani.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ameshtushwa na ajali hiyo. Aliwaambia waandishi wa habari mjini Berlin kwamba habari za kushtusha "zimetufikia kutoka kusini mwa Ufaransa." Bibi Merkel amesema kuanguka ndege ya abiria ya Ujerumani,kumesababisha msiba mkubwa kwa Ujerumani, Uhispania na Ufaransa. Ameeleza kuwa wamekubaliana kusaidiana ili kukijua kilichosababisha ajali ya ndege hiyo.

Waziri Steinmeier aenda kwenye sehemu ya ajali

Wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani imeunda kitengo maalumu kitakachoziratibisha shughuli zote zinazohusiana na ajali ya ndege iliyoanguka . Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier na mwenzake wa usafirishaji wanaelekea nchini Ufaransa. Kansela Angela Merkel amesema yeye pia ataenda Ufaransa kesho ili kupata habari zaidi juu ya ajali ya ndege hiyo.

Germanwings Airbus A320 abgestürzt PK Frank-Walter Steinmeier
Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Frank-Walter SteinmeierPicha: picture-alliance/dpa/B.v. Jutrczenka

Msemaji wa shirika la anga la Ufaransa ameeleza kwamba ndege ya abiria ya Ujerumani ilianguka karibu na mji wa Barcelonette umbali wa kilometa 100 kaskazini ya mji wa Nice. Habari zaidi zinasema ndege hiyo imeangukia mahala ambapo ni vigumu kupafikia kwa usafiri wa barabara.

Ndege ilishatumika kwa miaka 24

Ndege hiyo chapa ya A 320 ya shirika tanzu la Germanwings ilikuwa imeshatoa huduma kwa muda wa miaka 24 na ilikuwamo katika shirika mama la Lufthansa tokea mwaka wa 1991 .Shirika hilo tanzu limetoa salamu za rambi rambi kwa ndugu na jamaa waliofikwa na msiba.

Abiria 45 walikuwamo katika ndege hiyo walikuwa na majina yenye ubini wa kihispania. Na msemaji wa mji wa Haltern wa Ujerumani ameeleza kuwa ipo sababu ya kuamini kwamba watoto wa shule 16 na waalimu wawili kutoka mji huo wa Ujerumani walikuwamo katika ndege hiyo. Hata hivyo maelezo hayo hayajathibitishwa. Abiria 67 katika ndege hiyo walikuwa Wajerumani.

Mwandishi:mtullya abdu.

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman