1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NEC yashughulikia pingamizi 100 kati ya 500

11 Septemba 2020

Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini Tanzania (NEC) inasema hadi sasa imeshashughulikia rufaa zaidi ya 100 kazi ya 500 ambazo ziliwasilishwa kwake na wagombea waliopinga hatua ya kuondolewa kuwania ubunge na udiwani.

https://p.dw.com/p/3iKeN
Wahlen in Tansania I  Hamida Abdallah Huaeshi I Semistocles Kaijage I Hamida Abdallah Huaeshi
Picha: DW/S. Khamis

NEC inasema hadi sasa rufaa zilizosikilizwa na kutolewa maamuzi ni 111 za ubunge, huku 45 zikiwa ni za udiwani zilizowasilishwa na warufani walioenguliwa katika kinyang’anyiro cha uchaguzi na wasimamizi wa uchaguzi katika maeneo husika kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo hitalafu katika ujazaji wa fomu zao.

"Tumefaulu kuzipitia rufaa 111 katika nafasi ya ubunge na 45 katika nafasi ya udiwani na tunaendelea na zoezi huku wakiwajulisha warufani kadri matokeo yanavyotoka ili waweze kuendelea na mchakato wa uchaguzi," alisema Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Charles Mahera.

Tangu kuanza kutolewa kwa maamuzi ya rufaa hizo inakadiriwa kuwa zaidi ya rufaa 30 za nafasi ya ubunge zimefaulu kurejea katika kinyanga’anyiro cha uchaguzi huku taarifa ya hivi karibuni ikionesha rufaa 26 za nafasi ya udiwani zikikubaliwa na tume hiyo ya uchaguzi ambayo ilikuwa inaendelea na zoezi la kusikiliza rufaa zilizowasilishwa.

Upinzani walalamika

Tansania Dodoma Präsidentschaftskandidaten  ACT-Wazalendo-Partei Bernard Membe (R) und Omary Fakiy
Mgombea urais wa Tanzania kupitia ACT-Wazalendo, Benard Membe (kulia) na mgombea wake mwenza, Omar Faki Hamad, baada ya kukabidhiwa fomu za uteuzi na Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Tanzania (NEC).Picha: Tanzania National Electoral Commission NEC

Itakumbukwa kuwa tume hiyo iliwahi kuweka hadharani idadi ya rufaa zilizowasilishwa na warufani zikiwa ni takribani 500, ambazo zinatakiwa kusikilizwa kabla ya kuingia kwenye uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28, ambapo tayari kampeni zimekwishaanza kurindima katika maeneo mbalimbalii ya nchi.

Kabla NEC kuanza kupitia rufaa hizo mara kadhaa vyama vya upinzani vilitoka hadharani na kutoa malalamiko yao dhidi ya wasimamizi wa uchaguzi kuwakata wagombea wao kwa kile kilichotajwa kuwa kutokidhi vigezo vya uchaguzi.

Hata hivyo, baadhi ya vyama vya upinzani vinasema sasa wagombea wao wamerejeshwa, miongoni mwao ni chama cha ADC, ambacho katibu mkuu wake, Doyo Hassan, aliiambia DW kwamba wagombea 22 wa chama hicho waliokuwa wameondolewa, sasa wamerejeshwa.

Kwa kiasi kikubwa kadhia hii ya kuenguliwa haikuwagusa wagombea hawakukumbwa na madhila ya kuenguliwa katika uchaguzi huo, jambo ambalo lilidaiwa na vya vya upinzani kuwa huenda njama na hila za uchaguzi zilishika hatamu katika zoezi hilo la kidemokrasia. 

Imeandikwa na Hawa Bihoga, DW Dar es Salaam