1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Historia

Nelson Mandela, baba wa demokrasia Afrika

Sylvia Mwehozi
13 Februari 2020

Nelson Mandela ni moja kati ya wapigania uhuru nguli wanaopendwa Afrika. Alitumikia kifungo cha miaka 27 jela, na baadaye kuwa Rais wa kwanza mweusi wa Afrika ya kusini. Alisaidia kuiongoza nchi yake, kutoka kwenye siasa za ubaguzi wa rangi kuwa za kidemokrasia.

https://p.dw.com/p/2wFL4

Mandela aliishi wapi na lini? 

Alizaliwa katika eneo la milimani la Transkei, nchini Afrika Kusini mwaka 1918. Mandela alikwenda kusomea sheria katika Chuo Kikuu cha Fort Hare nchini humo. Mwaka 1944, alijiunga na chama cha siasa cha African National Congress, kilichoundwa kwa lengo la kukabiliana na sera za ubaguzi wa rangi za serikali ya wachache ya nchini Afrika Kusini iliyoongozwa na watu weupe. 

Na baadaye, mfumo huu ukabadilika na kuwa mapambano ya muda mrefu dhidi ya ubaguzi yaliyoongozwa na Mandela. Alikuwa rais wa kwanza wa Afrika Kusini, baada ya kukomeshwa kwa utawala wa kibaguzi, na alistaafu baada ya miaka mitano. Nelson Mandela alifariki Disemba 5, 2013, akiwa na miaka 95.
 
Nelson Mandela alijulikana kwa lipi? 

Nelson Mandela aliunda tawi la kijeshi ndani ya ANC lililojulikana kama "Umkhonto we Sizwe" au "Mkuki wa taifa" ili kukabiliana na serikali iliyoko mamlakani na sera zao za ubaguzi wa rangi. Alishitakiwa kwa hujuma na kupanga njama za kuipindua serikali mnamo mwaka 1964, na ndipo alipofungwa kifungo cha maisha katika gereza lililopo kwenye kisiwa cha Robben, ambako alitumikia kifungo kwa miaka 27. Baada ya kuachiwa mwaka 1990, Mandela alikuwa rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini, mwaka 1994.

Nelson Mandela aliweza kumudu kifungo kirefu gerezani? 

Mandela alikivutia kizazi cha Afrika Kusini kwa kuwa ingawa alikuwa kifungoni kwa muda mrefu, utu wake na mtizamo wake juu ya ulimwengu ulipenya hadi nje ya kuta za gereza. Miongo kadhaa aliyotumikia kifungo haikumvunja nguvu, bali ilimjengea mchango wake wa kihistoria katika mapambano ya kusaka uhuru wa taifa hilo. Baadhi ya nyimbo za kupinga ubaguzi wa rangi zilitoa mwito wa kuachiwa huru kwa Nelson Mandela, na miongoni mwa nyimbo hizo ni ule wa Johnny Clegg na Savuka ulioitwa, "Asimbonanga" ukiwa na maana "Hatujamuona".

African Roots Nelson Mandela
Picha: Comic Republic

Nelson Mandela anaheshimika kwa lipi? 

Licha ya miaka kadhaa ya ugumu na kifungo, Mandela hakuwahi kupoteza maono yake kuhusu amani, jamii iliyo na usawa nchini Afrika Kusini na nafasi yake katika kulitumikia taifa lake. Aliamini katika taifa la kidemokrasia, ambalo kila raia anakuwa na haki ya kupiga kura. Aliiongoza Afrika Kusini kwa awamu moja, na kufungua njia kwa raia kushiriki haki ya kidemokrasia ya kuchagua kiongozi atakayefuata, kuliongoza taifa hilo.

Alitunukiwa tuzo ya amani ya Nobeli mwaka 1993, pamoja na rais wa zamani wa taifa hilo, F.W. de Klerk. De Klerk, awali aliondoa zuio la chama cha ANC na kumuachia huru Nelson Mandela kutoka kifungoni. kwa pamoja walishirikiana kuliondoa taifa hilo kutoka katika utawala wa kibaguzi.

Nukuu zipi maarufu zilitumiwa na Nelson Mandela?

Alipozungumzia kesi yake mwaka 1964:  alisema "nimepambana dhidi ya utawala wa weupe, na nimepambana dhidi ya utawala wa weusi. Ninathamini wazo la jamii ya kidemokrasia na jamii iliyo huru ambayo watu wote wataishi pamoja kwa maelewano na fursa sawa. Ni wazo ambalo natumai kulisimamia na kuhakikisha kuwa linatimia. Lakini ikibidi, ni wazo ambalo niko tayari kufa nikilitetea"

"Mara zote huonekana kama hakiwezekani, hadi pale kitakapofanyika."

"Elimu ni silaha yenye nguvu zaidi ambayo unaweza kutumia kuibadilisha dunia."

"Nimejifunza kwamba ujasiri haumaanishi kuwa hakuna hofu, lakini ni ushindi dhidi yake. Mtu jasiri sio yule ambaye hatishiki, lakini ni yule anayeshinda."

Kutana na Nelson Mandela

Ni urithi upi aliouacha Nelson Mandela? 

Kwa kizazi cha sasa cha Afrika Kusini, Mandela ameacha urithi wa kujitoa na kutokuwa na mashaka katika kupambania haki za binaadamu kwa wote. Maono yake kwa ajili ya taifa hilo la Afrika Kusini kuwa watu weusi  na weupe wangeweza kuishi kwa usawa bila ya kutengwa huenda hayakutimia kikamilifu, lakini utawala wake ulifanikiwa katika kuipigia debe itikadi hiyo bila kujali ugumu wake katika jukwaa la kisiasa.

Victoria Averill, Thuso Khumalo na Gwendolin Hilse walichangia katika makala hii. Ni sehemu ya mfululizo wa makala maalumu za DW "Asili ya Afrika", zinazoangazia historia ya Afrika, kwa ushirikiano na Shirika la Gerda Henkel .

Mwandishi: Averill, Victoria
Tafsiri: Mtono, Lillian
Mhariri: Yusuf Saumu