Netanyahu asimamishwa kizimbani tuhuma za ufisadi
10 Desemba 2024Ni mara ya kwanza kwa waziri mkuu wa Israel kusimamishwa kizimbani akikabiliwa na makosa ya jinai, ikiwa ni hatua ya kufedhehesha kwa kiongozi ambaye mara zote amekuwa akiweka taswira ya kuwa yeye ni mwanasiasa makini, mahiri na kiongozi wa kuheshimika.
Netanyahu, mwenye umri wa miaka 75, anajibu mashtaka ya udanganyifu, kuvunja uaminifu na kupokea rushwa katika kesi tatu tofauti zinazomkabili.
Anatuhumiwa kwa kupokea maelfu ya dola za kimarekani, sigara na mvinyo wa bei ghali aina ya 'champagne' kutoka kwa bilionea mmoja mtayarishaji wa filamu wa Hollywood kwa makubaliano kwamba Netanyahu angelimsaidia katika mambo ya kibinafsi na ya kibiashara.
Aidha, anakabiliwa pia na mashtaka yanayohusiana na kuendeleza udhibiti unaowanufaisha matajiri wa vyombo vya Habari kwa makubaliano kwamba magwiji hao watampa Netanyahu nafasi ya juu kwenye vyombo vya habari pamoja na familia yake.
Waziri Mkuu huyo wa Israel anakanusha kufanya makosa, akisema mashtaka hayo ni njama ya kumchafua kisiasa.