1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NEW YORK: Annan aeleza wasiwasi mkubwa juu ya waafrika wahamiaji

8 Oktoba 2005
https://p.dw.com/p/CETo

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa bwana Kofi Annan ameeleza wasi wasi mkubwa juu ya hali mbaya inayowakabili waafrika waliojaribu kuhamia nchini Uhispania kwa kupitia Morocco.

Bwana Annan ameeleza wasi wasi huo kufuatia vifo vya waafrika sita waliojaribu kuruka uzio wa seng’enge ili kuingia Uhispania.

Katibu Mkuu Annan amezisihi serikali za Morocco na Uhispania zishughulikie mkasa wa waafrika hao kwa moyo wa kiutu.

Habari zaidi zinasema kwamba wajumbe wa Umoja wa Ulaya na Umoja wa Mataifa wanaelekea nchini Morocco ili kuona jinsi idara za nchi hiyo zinavyowashughulikia waafrika 73 waliorudishwa kwa nguvu nchini Morocco baada ya kukataliwa kuhamia nchini Uhispania.

Shirika la misaada la madaktari mipaka wazi pia limeripoti kwamba limewaona waafrika zaidi ya mia tano waliotelekezwa jangwani na polisi wa Morocco bila ya chakula wala maji.