NEW YORK : Annan ashutumu ukiukaji wa makubaliano na Israel
20 Agosti 2006Katibu Mkuu wa Umoja was Mataifa Kofi Annan amesema hapo jana Israel imekiuka makubaliano ya Umoja wa Mataifa ya kusitisha mapigano nchini Lebanon na kuzitaka pande mbili husika kuheshimu kuzuwiya upelekaji wa silaha bila kibali nchini Lebanon.
Taarifa iliyotolewa na msemaji wa Annan imesema Katibu Mkuu ana wasi wasi mkubwa juu ya ukiukaji uliofanywa na upande wa Israel wa kusitisha uhasama kama ilivyotajwa katika azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa nambari 1701.
Makamandoo wa Israel walishambulia ngome muhimu ya Hezbollah ndani kabisa nchini Lebanon hapo jana na kupambana vikali na wapiganaji wa kundi hilo.Israel imesema shambulio hilo lilofanywa kuzuwia usafirishaji wa silaha wa magendo kutoka Iran na Syria kuwapelekea wanamgambo wa Kishia wa kundi la Hizbollah limepelekea kuuwawa kwa mwanajeshi mmoja wa Israel na wengine wawili kujeruhiwa.Pia imeripotiwa kwamba wapiganaji watatu wa Hizbollah wameuwawa.
Serikali ya Lebanon imetishia kusitisha uwekaji zaidi wa wanajeshi wake kusini mwa Lebanon kupinga shambulio hilo la Israel wakati makubaliano ya kusitisha mapigano ya Umoja wa Mataifa yaliodumu kwa siku sita sasa yakiwa katika mtihani mgumu.