NEW YORK : Annan ataka mkakati wa silaha za maangamizi
21 Novemba 2006Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan ameitaka jumuiya ya kimataifa kuandaa mkakati kabambe kuhakikisha kwamba silaha za maangamizi makubwa ikiwa ni pamoja na silaha za kibiolojia haziishii mikononi mwa magaidi.
Akizungumza katika kikao cha ufunguzi cha Mkutano wa Sita wa Tathmini ya Makubaliano ya Silaha za Kibiolojia mjini Geneva amesema kwa hakika wanahitaji kushughulikia ukomeshaji na kuzuwiya kuenea kwa silaha za nuklea kwa kuzingatia misingi ya makubaliano ya kuzuwiya kuenea kwa silaha hizo.
Annan ameongeza kusema kwamba lazima washughulikie suala la ugaidi na uhalifu katika ngazi isio ya kitaifa na ya kibinafsi kwa kupambana na suala hilo kwa kujumuisha afya ya jamii, misaada ya maafa na juhudi za kuhakikisha kwamba matumizi ya amani ya sayansi ya biolojia na teknolojia yanaweza kuwafikia kwa usalama wahusika waliokusudiwa.