1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NEW YORK: Katibu Mkuu mpya wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon kulipa kipaumbele suala la Darfur.

3 Januari 2007
https://p.dw.com/p/CCdh

Katibu Mkuu mpya wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, amesema ameamua kulipatia kipaumbele suala la mzozo wa Darfur nchini Sudan

Ban Ki-Moon alikuwa akizungumza kutoka makao makuu ya Umoja huo mjini New York siku yake ya kwanza kuwa afisini.

Katibu Mkuu huyo amesema angependa kushiriki katika kikao cha Umoja wa Afrika cha mwishoni mwa mwezi huu mjini Addis Ababa, Ethiopia, na kushauriana na Rais wa Sudan, Omar Hassan Al-Bashir.

Sudan imekuwa ikipinga kupelekwa majeshi ya Umoja huo ya kulinda amani katika eneo hilo lenye mzozo.

Ban Ki-Moon pia alizungumzia uamuzi wa serikali ya Iraq kumnyonga Saddam Hussein akisema suala la hukumu ya adhabu ya kifo ni la mataifa wanachama kuamua yanavyotaka kutekeleza sheria zake.

Ban Ki-Moon alisema:
"Kila taifa mwanachama lina haki ya kuamua jinsi ya kutekeleza sheria zake hasa linapozungumziwa suala la adhabu ya kifo. Ninapinga sana hali ya kutowajibika lakini ningetaka jumuiya ya kimataifa kuheshimu vipengee vyote vya sheria za kimataifa kuhusu haki za binadamu"

Katibu Mkuu huyo ameahidi atahakikisha usawa wa kijinsia na kijiographia wakati wa kutoa ajira za Umoja huo sio tu katika makao makuu ya New york bali pia katika afisi za nyanjani.