1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

New York. Wanaofanya biashara ya dhahabu kuchunguzwa.

14 Julai 2007
https://p.dw.com/p/CBiu

Umoja wa mataifa umesema kuwa utaharakisha upelekaji wa kikosi cha uchunguzi cha umoja wa mataifa katika jamhuri ya kidemokrasi ya Congo ili kuchunguza madai ya biashara ya dhahabu inayofanywa na baadhi ya wanajeshi wake katika jeshi la kulinda amani nchini humo.

Madai hayo yanawahusu wanajeshi wa kulinda amani kutoka India nchini Congo, wanaotuhumiwa kufanya biashara ya kubadilishana kwa chakula na hata taarifa za kijeshi na waasi wa Kihutu wa Rwanda, ili kupata dhahabu.

Uchunguzi huo ni moja kati ya hatua kadha zinazochukuliwa katika ujumbe huo wenye wanajeshi 17,000 wa umoja wa mataifa katika jamhuri ya kidemokrasi ya Congo.

Operesheni hiyo imesifiwa kwa kuwezesha kufanyika kwa uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia nchini humo katika muda wa miaka 40 lakini imetiwa doa na tuhuma kadha ambazo ni pamoja na kashfa za vitendo vya ngono pamoja na mauaji.

Wanaharakati wanaotetea haki za binadamu wameeleza wasi wasi wao kuwa kashfa hizo zinaweza kuchafua sifa ya ujumbe wa kulinda amani wa umoja wa mataifa.