1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ni kiza kinene Gaza!

Admin.WagnerD19 Novemba 2012

Raia wa Palestina mjini Gaza wanazidi kuteketezwa kwa mashambulizi ya Israel ambapo asubuhi ya Jumatatu tu wapalestina 17 wameuawa na kufikisha jumla ya vifo 94 tangu kuanza kwa mashambulizi hayo siku sita zilizopita.

https://p.dw.com/p/16lTv
Wanajeshi wa israel wakiandaa kifaru katika mpaka na Gaza.
Wanajeshi wa israel wakiandaa kifaru katika mpaka na Gaza.Picha: Reuters

Wakati vurugu zikiongezeka, juhudi za kimataifa za kusitisha mapigano nazo zimeshika kasi, ambapo afisa mwandamizi wa chama cha Hamas aliyeko Misri amesema mazungumzo na Israel yaliyoratibiwa na Misri yalikuwa na matokeo mazuri, lakini sasa hivi yamejikita katika kujadili masharti ya makubaliano. Ofisi ya rais Mohammed Mursi ilisema rais huyo alikutana na kiongozi wa Hamas Khaled Meshaal na kiongozi wa kundi la Islamic Jihad Abdullah Shalah, kujadili juhudi za Misri kukomesha uvamizi.

Mwanamke wa Kipalestina akitizama uharibifu uliyofanywa dhidi ya makaazi yake.
Mwanamke wa Kipalestina akitizama uharibifu uliyofanywa dhidi ya makaazi yake.Picha: Reuters

"Juhudi za majadiliano zinafanyika kati ya Israel na Hamas kupitia njia mbalimbali, na kuna ushahidi wa uwezekano wa kusitisha mapigano kati ya pande mbili. Lakini mpaka sasa hakuna uhakika, lakini nataka kubainisha na kusisitiza kwamba si vita, wala uvamizi wa aina hii na kuzingirwa kwa Gaza vitaleta amani na utulivu kwa watu wa kanda hii," alisema rais Mursi

Ban Ki-Moon aunga mkono juhudi za Misri

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon amewataka Hamas na Israel kushirikiana na Misri ili kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano, na katika taarifa yake amesema anaelelekea kwenye eneo hilo kuunga mkono juhudi za amani. Ofisi yake haikusema ni lini atawasili lakini wizara ya mambo ya kigeni ya Israel imesema inamtegemea siku ya Jumatano, na mamlaka ya Palestina nayo ikithibitisha kuwa atakutana na rais wa mamlaka hiyo Mahmoud Abbas siku hiyo.

Rais wa Israel, Shimon Perez amesema nchi yake haitaki vita na Hamas lakini hawana njia nyingine. "Hatuna nia ya kuingia vitani na Hamas, na wala hatutaki kuibadilisha Gaza, hatutaki kufanya mashambulizi yoyote lakini hatuna njia nyingine." Waziri wa mambo ya kigeni Avigdor Lieberman alisisitiza kuwa sharti la kwanza lisilo na mjadala ni kwa Hamas kusitisha mashambulizi yote kutoka Gaza, na kwamba makundi yote yenye silaha laazima yajifunge na masharti hayo.

Wanajeshi wa Israel wakiandaa vifaru katika kituo cha kijeshi karibu na mpaka wa nchi hiyo na Gaza.
Wanajeshi wa Israel wakiandaa vifaru katika kituo cha kijeshi karibu na mpaka wa nchi hiyo na Gaza.Picha: MENAHEM KAHANA/AFP/Getty Images

Hamas yataka kuondolewa kwa vizuizi vya Israel kwanza

Wachambuzi wanasema Israel imeridhika na operesheni hiyo na kwamba inaweza kuwa tayari kwa mazungumzo, lakini Hamas ambayo imepata kuungwa mkono na mataifa ya kiarabu, imetaka kama sharti moja wapo ya kusitisha mashambuli, kuondolewa kwa vizuizi vilivyowekwa na Israel mwaka 2006, na uthibitisho wa kimataifa, kwamba itasitisha mashambulizi yake dhidi ya Gaza, ikiwemo mauaji ya viongozi wa chama hicho. Vurugu za sasa zilianza kwa mauaji ya kiongozi wa tawi la kijeshi la Hamas, Ahmed Jabbaari katika shambulio la Israel mjini Gaza Jumatano wiki iliyopita.

Licha ya Israel kudai kuwa mashambulizi yake yanalenga vituo vya Hamas, wengi wa waliouawa katika mashambulizi hayo ni raia wa kawiada wakiwemo watoto. Vifo vya leo vimefuatia mashambulizi mfululizo siku ya Jumapili ambapo watu 29 waliuawa. Waisrael watatu ndiyo wameuawa tangu kuanza kwa mgogoro huo, na zaidi ya 50 wamejeruhiwa na mashambulizi ya roketi.

Jeshi la Israel limesema siku ya Jumatatu kuwa limefanikiwa kuvishambulia vituo visivyopungua 80 vya Hamas katika usiku moja, yakiwemo makao makuu ya Polisi ya Hamas, na kufikisha jumla ya vituo vilivyoshambuliwa kuwa 1,350. Msemaji wa jeshi la Israel alisema hakuna shambulio la roketi kutoka Gaza usiku wa kuamkia leo, ingawa yapo mawili yaliyoripuka mapema Jumatatu.

Katibu mkuu wa jumuiya ya nchi za Kiarabu Nabil al-Araby (kushoto) na waziri wa mambo ya kigeni wa Lebanon Adnan Mansour (katikati) wakihudhuria mkutano wa dharura mjini Cairo, Misri kuhusu vurugu zinazoendelea mjini Gaza. Araby alisema jumuiya hiyo itaangalia upya uhusiano wake na Israel kufuatia mgogoro huo.
Katibu mkuu wa jumuiya ya nchi za Kiarabu Nabil al-Araby (kushoto) na waziri wa mambo ya kigeni wa Lebanon Adnan Mansour (katikati) wakihudhuria mkutano wa dharura mjini Cairo, Misri kuhusu vurugu zinazoendelea mjini Gaza. Araby alisema jumuiya hiyo itaangalia upya uhusiano wake na Israel kufuatia mgogoro huo.Picha: Mahmud Khaled/AFP/Getty Images

Miongoni mwa waliyouawa siku ya Jumatatu ni wakulima watatu, na wanafamilia watatu waliouawa katika shambulio dhidi ya gari katika eneo la Deir al-Balah katikati ya Gaza. Mjini Gaza kwenyewe, wanawake wawili na mtoto walikuwa miongoni mwa watu wanne waliyouawa katika shambulio dhidi ya eneo la Zeitun.

Uingereza yaitahadharisha Israel

Waziri mkuu Benjamini Netanyahu alionya siku ya Jumapili kuwa Israel iko tayari kupanua operesheni hiyo, huku kituo kimoja cha redio ya umma kikiripoti kuwa wanajeshi wa akiba elfu 40 walikuwa wamewekwa karibu na mpaka wa Gaza tayari kwa operesheni ya ardhini.

Rais wa Marekani Barack Obama alisema ni vizuri mgogoro huo ukamalizika bila Israel kupeleka majeshi yake mjini Gaza, wakati waziri wa mambo ya kigeni wa Ufaransa, Laurent Fabius akisema nchi yake iko tayari kusaidia katika usulihishi.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Uingereza William Hague.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Uingereza William Hague.Picha: AP

Kwa upande wake, waziri wa mambo ya kigeni wa Uingereza William Hague alionya kuwa operesheni ya ardhini ndani ya Gaza itaikosesha Israel uungwaji mkono kimataifa na huruma waliyo nayo sasa hivi, ikiwemo nchini Uingereza kwenyewe.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/afpe

Mhariri: Saum Yusuf Ramadhan