Ni lini Ujerumani itaiomba msamaha Namibia juu ya mauaji?
11 Juni 2020Katika hotuba yake kwa taifa wiki iliyopita, Rais Hage Geingob alidokeza kuwa Ujerumani inakaribia kuomba msamaha kwa mauaji ya maelfu ya watu wakati wa enzi ya ukoloni. "Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani imekubali kuwa matukio ya kati mwaka wa 1904 – 1908 yanaweza kutambulika kama mauaji ya halaiki na wako tayari kuomba msamaha, katika kiwango cha juu kabisa cha serikali.” Geingob aliwaambia wabunge Juni 4.
Gazeti linalomilikiwa na serikali ya Namibia la New Era likaandika siku iliyofuata kuwa "Hatimaye Ujerumani kuomba msamaha kwa mauaji ya halaiki”.
Ujerumani yakataa kuzungumzia
Mazungumzo ya faragha kati ya serikali hizo mbili yalianza 2015 baada ya Ujerumani kukataa kwa miongo mingi kukubali kuwa mauaji ya maelfu ya watu wa Herero na Nama katika koloni hilo la zamani la Ujerumani yalikuwa mauaji ya halaiki.
Serikali ya Ujerumani ilikataa kuzungumzia kauli hiyo ya rais wa Namibia. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Kigeni Christofer Burger aliwaambia wanahabari mjini Berlin kuwa;
"Mazungumzo yanaendelea katika mazingira ya pande zote kuaminiana. Pande zote mbili zimekubaliana kuhusu usiri na ndio maana hawazungumzii hatua zilizopigwa wala yanayozugumzwa, lakini narudia tena nilichosema zamani kuwa lengo la mazungumzo haya ni kumalizika kwa ombi la msamaha. lakini pia katika njia ambayo upande wa Namibia utaridhia."
Ujerumani mara nyingi imeahidi kutangaza rasmi ombi la msamaha kwa mauaji hayo ya enzi za ukoloni. Ruprecht Polenz, mjumbe wa Ujerumani katika mazungumzo hayo na Namibia, alisema Februari kuwa serikali hizo mbili zinakaribia kukubaliana kuhusu tamko la pamoja kuhusu mauaji hayo.
Ujerumani daima imefuta uwezekano wa kulipa fidia kwa mauaji hayo. Badala yake, serikali imejitolea kufadhili miradi ya ziada ya maendeleo katika maeneo ambayo Waherero na Wanama wanaishi.
Mzozo kuhusu fidia
Hilo linaonekana kutochukuliwa vizuri kwa upande wa Namibia. Geingob alidai kuwa Ujerumani awali ilikubali kutoa euro milioni 10, kiasi ambacho aliona kuwa "tusi" kwa upande wa Namibia.
Katika hotuba yake kwa taifa, Geingob alikiri kuwa masuala ya kifedha hayajatatuliwa. "Kinachosalia sasa ni makubaliano ya mwisho ya maelezo na kiwango cha mpango wa maridhiano na ujenzi.” Alisema.
Ombi la msamaha kutoka kwa Ujerumani hata hivyo linaonekana kutowezekana kama suala la kifedha halitakuwa limekubaliwa na pande zote.
Ishara kwa Ujerumani na Namibia
Waangalizi wanaamini kuwa Geingob huenda amechagua kuonyesha hatua za mazungumzo hayo katika mtazamo chanya ili kuisafisha picha ya serikali yake. Dietrich Remmert, mchambuzi kutoka Taasisi ya Utafiti wa Sera ya Umma mjini Windhoek – IPPR ameiambia DW kuwa uchumi wa Namibia bado unayumba tangu mporomoko wa mwaka wa 2016. Umepata pigo jingine kutokana na janga la COVID-19. Nadhani alikuwa pia akijaribu kutafuta vitu vizuri ambavyo angeweza kutangaza kwa taifa.
Kauli ya Rais huenda pia ilikuwa ni jaribio la kuwasiliana na Waherero na Wanama. Baadhi ya viongozi wa jadi wanatofautiana na serikali kuhusu suala hilo. Wanadai mazungumzo ya moja kwa moja na serikali na kuituhumu serikali ya Namibia kwa kushindwa kuwakilisha maslahi yao.
Mwisho matamshi ya Geingob huenda pia yalielekezwa kwa serikali ya Ujerumani. Remmert kutoka IPPR anasema wachambuzi kadhaa nchini Namibia wanasema kisiri kuwa kujikokota kwa mazungumzo ni kitu ambacho kinaweza kulaumiwa kwa upande wa Namibia, kwa kutojiandaa vya kutosha na kwa kuzembea kushiriki katika mazungumzo hayo.
Hivyo basi bado haijulikani ni lini serikali hizo mbili huenda zikafikia makubaliano ya mwisho. Duru mpya ya mazungumzo iliyokuwa imepangwa Machi iliahirishwa kutokana na janga la COVID-19, lakini mazungumzo yanasemekana kuendelea katika kiwango cha jopokazi. Serikali ya Ujerumani imesema mara kwa mara kuwa inatumai mazungumzo hayo yatakamalika haraka iwezekanavyo.