1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahanga wa ajali ya ndege ya MH17 wakumbukwa

17 Julai 2015

Jamaa za wahanga wa ajali ya ndege ya Malaysia ya MH17 iliyodunguliwa mashariki ya Ukraine mwaka jana wamekusanyika hii leo kwa ibada ya makumbusho nchini Australia na Uholanzi.

https://p.dw.com/p/1G0QN
Picha: picture-alliance/dpa/F. Ismail

Mnamo tarehe 17 mwezi Julai mwaka jana; ndege ya shirika la ndege la Malaysia nambari MH17 iliyokuwa na watu 298 ikitokea Amsterdam kuelekea Kuala Lumpur ilidunguliwa mashariki ya Ukraine. Abiria wote na wahudumu waliokuwa katika ndege hiyo waliuawa.

Miongoni mwa wahanga wa ajali hiyo walikuwa ni abiria 38 wa Australia. Wengi wa waathiriwa hata hivyo walikuwa ni raia wa Uholanzi. Hii leo waziri mkuu wa Australia Tony Abbott amezindua makumbusho ya kudumu yaliyo na majina ya waliouawa kuwakumbuka waathiriwa wa mkasa huo mjini Canberra.

Abbott na mkewe wameweka shada la maua katika makumbusho hayo wakifuatiwa na jamaa za waathiriwa ambao bado wana majonzi. Mapema hii leo, waziri wa mambo ya nje wa Australia Julie Bishop amesema ametiwa kichefuchefu na kutolewa kwa vidio mpya katika vituo vya habari nchini humo inayoonyesha waasi wa mashariki ya Ukraine wakipekua mizigo ya abiria wa ndege hiyo iliyoangushwa.

Haki bado haijatendeka mwaka mmoja baadaye

Abbott amesema vidio hiyo inadhihiridha kuwa ndege hiyo ilidunguliwa kimakusudi na waasi hao. Australia, Ubelgiji, Malaysia, Uholanzi na Ukraine zimelitaka baraza la usalama la umoja wa Mataifa kuunda mahakama maalumu ya uhalifu kuwashitaki waliohusika katika udunguaji huo wa ndege hiyo ya Malaysia.

Jamaa za waathiriwa wakiweka mashada ya maua Australia
Jamaa za waathiriwa wakiweka mashada ya maua AustraliaPicha: picture-alliance/AP Photo/D. Gray

Serikali ya Ukraine inawashtumu waasi wanaotaka kujitenga kwa eneo la mashariki ya Ukraine kwa udunguaji huo huku Urusi ambayo inawaunga mkono waasi hao ikiishutumu serikali ya Ukraine kwa kuhusika.

Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza Philiph Hammond ametaka kuundwa kwa mahakama maalumu inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa kuwashitaki waliohusika katika kuidungua ndege ya abiria ya shirika la Malaysia nambari MH17 mwaka jana nchini Ukraine.

Hammond ambaye nchi yake ni mwanachama wa kudumu wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa amesema haki sharti itendeke kwa wahanga 298 waliokufa katika ajali hiyo na ili hilo liwezekane, mahakama maalumu inahitajika kuundwa baada ya kupitishwa kwa azimio na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kuwafungulia mashitaka waliohusika.

Urusi yapinga kuundwa kwa mahakama maalum

Rais wa Urusi Vladimir Putin ambaye pia nchi yake ni mwanachama wa kudumu wa baraza la usalama amemwambia Waziri mkuu wa Uholanzi Mark Rutte kuwa kuundwa kwa mahakama hiyo hakutakuwa na tija.

Mabaki ya ndege ya MH17
Mabaki ya ndege ya MH17Picha: Oleg Vtulkin

Uholanzi ndiyo iliyo na wajibu wa kuongoza uchunguzi wa kubaini kilichosababisha ajali hiyo na kuitambua miili ya waathiriwa pamoja na kuwatambua na kuwaadhibu waliohusika.

Shirika la kusimamia usalama wa safari za ndege la Uholanzi linatarajiwa kutoa ripoti kamili kuhusu ajali hiyo mwanzo mwa mwezi Oktoba. Baraza la usalama liliidhinisha azimio nambari 2166 linalotaka waliohusika kufunguliwa mashitaka na kwamba nchi zote zishirikiane kikamilifu katika juhudi za kutambua uwajibikaji.

Bendera zitapeperushwa nusu mlingoti hii leo nchini Uholanzi huku kiasi ya jamaa elfu mbili wa wahanga wakikusanyika kuwakumbuka wapendwa wao na ibada ya kitaifa ya makumbusho itafanyika.

Mwandishi:Caro Robi/afp/dpa

Mhariri: Josephat Charo