Ni nini unaweza kufanyia hizo fedha?
Msimu wa soka 2017/18 umeanza. Kwa mashabiki wengi, kipindi kirefu cha njaa kimefikia mwisho, lakini kwa vilabu vingi, kengele za fedha zinaanza kulia. Hakujawahi kuwa na fedha nyingi katika soka kama ilivyo sasa.
Poromoko la fedha
Ni dhahiri kuwa euro milioni 222 za uhamisho zilisaidia kumshawishi Neymar da Silva Santos Jr. kufanya uamuzi kuwa kucheza soka karibu na mnara wa Eiffel kunachangamsha zaidi kuliko akiwa Barcelona. Mbrazil huyo anaondoka Uhispania kuelekea Ufaransa kwa sababu sheikh mmoja kutoka Mashariki ya Kati alikubali kutoa kitita kikubwa mfukoni - huo ni utandawazi!
Kufuata fedha…
... kwa mfano katika klabu ya Dortmund: Mamilioni ya euro zilizolipwa kwa uhamisho wa Neymer hazikuwa zimefika Barcelona wakati Barca ilipotuma ujumbe maalum nchini Ujerumani kujaribu kumshawishi mchezaji mwenye kipaji Ousmane Dembele kwamba atalipwa fedha nyingi nchini Uhispania kuliko akiwa Borussia Dortmund. (Lakini kama si sasa, basi labda katika msimu wa baridi?)
Kutumia fedha kwa njia huru
Hata hivyo wale wanaolalamika kuhusu viwango vya juu vya malipo ya uhamisho wa wachezaji, hawapaswi tu kuwalaumu Waarabu, Wachina au Warusi. Timu za Bundesliga pia zimechangia hali hiyo: Hivi karibuni Borussia Dortmund iliilipa Freiburg euro milioni 20 kumsajili mshambuliaji Maximilian Philipp. Kulingana na viwango vya Ujerumani, japo Philipp anacho kipaji, tayari ni mchezaji ghali.
Mwisho wa vyote ni kuwa 'fedha nyingi' hutegemea mambo mengi
Lakini je wachezaji hawa wenye mwendo wa kasi wanalipwa hela ngapi? Ni suala ambalo Bundesliga imeweka siri. Lakini, fununu zinasema kuwa katika mwaka, Neymar atalipwa euro milioni 30. Tukichanganua ni kuwa: kwa wastani, mkuu wa kampuni ya DAX ya Ujerumani hulipwa takriban milioni 6.4 na mchezaji wa Bundesliga hulipwa euro milioni 1.9. Shabiki kwa upande mwingine hupata takriban euro 42, 000.
Haiishii hapo
Wachezaji wa timu 18 za Bundesliga, hugharimu vilabu vyao takriban euro milioni 75. Ligi ya Uingereza hutumia zaidi ya kiwango hicho maradufu, - euro milioni 152 kuhakikisha wachezaji wanavutiwa kucheza katika ligi hiyo. Lakini mshahara wa Neymar wa euro milioni 30, utabadili hali.
Wadhamini wakubwa na wadogo
Fedha za wachezaji hazitoki tu kwa wadhamini wakubwa. Pia hutoka kwa mashabiki. Shabiki mmoja wa HSV Hamburg anaweza kulipa euro 800 kununua tiketi katika msimu mmoja, licha ya kuwa timu inaweza kushushwa daraja. Pia mashabiki hununua jezi ya klabu inapocheza nyumbani na inapocheza ugenini. Pamoja na vifaa vingine vyenye nembo ya timu huleta fedha.
Uhuru-kwa-wote
Katika Bundesliga, mfumo ujulikanao kama 50+1 ni sheria kwa takriban timu zote. Sheria hii inalenga kuwazuia matajiri wa Urusi na China au Uarabuni kuingia Ujerumani na kununua kilabu kizima. Lakini timu ya Hannover 96 imepuuzilia mfumo huo. Rais wa timu hiyo Martin Kind anafikiri hali haitakuwa mbaya sana.
Kushinda mechi kutumia fedha
Wengi wanaamini kuwa Bayern Munich watashinda ligi tena. Timu hii ndiyo yenye thamani ya juu zaidi katika ligi, takriban euro bilioni 2.4. Kilicho wazi ni kuwa Dortmund na Schalke hawawezi kufikia kiwango hicho. Kwa jumla thamani ya Schalke na Borrusia Dortmund zikiwekwa pamoja ni euro bilioni 1.7.
Cristiano Ronaldo, Gareth Bale na Paul Pogba: Wote walisajiliwa kwa fedha nyingi au takriban euro milioni 100 kila mmoja kama ada ya uhamisho. Wengi wamesema kuwa hilo halikubaliki. Lakini ghafla hali imefikia kiwango tofauti kutokana na kiasi cha fedha ambacho Neymar alinunuliwa. Kwa sasa hakika hata Bundesliga itahisi athari zake.