1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ni siku ya kimataifa ya kukabiliana na dawa za kulevya

Admin.WagnerD26 Juni 2013

Leo ni siku ya kimataifa ya kupambana na dawa za kulevya na biashara haramu ya dawa hizo. Umoja wa Mataifa umeitenga siku hii kuuhimiza ulimwengu kupambana na janga hili ambalo linaathiri hasa vijana kote duniani.

https://p.dw.com/p/18wl7
Picha: picture alliance/dpa

Afisi ya Umoja wa Mataifa inayokabiliana na dawa za kulevya na uhalifu, UNODC, imesema hapo jana mjini Vienna, Austria, kuwa kuna aina mpya ya dawa za kulevya ambazo zinaepuka marufuku zinazotambulika na zinatengezwa kwa kiwango cha juu mno kiasi ya kukipiku kiwango cha dawa za kulevya zilizoharamishwa.

Ripoti inayotolewa kila mwaka na shirika hilo la UNODC imesema athari za dawa hizo mpya zinafanana na zile kama za amphetamine, bhangi na miraa lakini zinaweza kuwa hatari zaidi kwani hakuna taarifa za kutosha kuhusu madhara na uraibu wake.

Mraibu wa dawa za kulevya akijidunga sindano
Mraibu wa dawa za kulevya akijidunga sindanoPicha: picture-alliance/dpa

Nchi kadhaa zimeripoti kwa shirika hilo aina 251 za dawa mpya kufikia katikati ya mwaka jana ambayo ni zaidi ya zile zilizopigwa marufuku chini ya mikataba ya kimataifa ambazo idadi yake ni 234.

Kuibuka kwa dawa mpya kwazua wasiwasi

Ripoti hiyo inasema kuwa imekuwa vigumu kwa serikali kote duniani kuzipiga marufuku hizi dawa mpya kwa sababu utaratibu unaotumika kuzitengeza si kama ule wa dawa zinazojulikana. Nyingi ya dawa hizi zinatengezwa barani Asia na Ulaya.

Katika nchi za Umoja wa Ulaya, mmoja kati ya vijana 20 ameshazijaribu dawa hizi mpya za kulevya ambazo mara nyingi huuzwa kama dawa za mitishamba au chumvi za kuogea.

Katika ujumbe wake wa kuadhimisha siku hii ya kukabiliana na dawa za kulevya, Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa, Ban ki Moon, amesema dawa za kulevya kote duniani zinatishia afya na maslahi ya vijana, watoto familia na jamii kwa ujumla na mabilioni ya fedha zinazotokana na biashara hii haramu zinakuza ufisadi, na kuyapa mitandao ya wahalifu nguvu zaidi na hivyo kuzua hofu na misukosuko.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban ki Moon
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban ki MoonPicha: Reuters

Ban ameongeza kusema kuwa biashara ya dawa za kulevya ni kikwazo kikubwa kwa maendeleo na kwamba tatizo hilo ambalo linamgusa kila mmoja linahitaji sheria madhubuti na shirikishi miongoni mwa nchi kwani ni jukumu la kila mmoja.

Ni jukumu la kila mmoja kupambana na dawa

Bado kiwango cha matumizi ya dawa kama vile Heroin, cocaine na amphetamine hakijashuka lakini mtindo huu wa kuwepo kwa aina mpya za dawa za kulevya unatia wasiwasi.

Takwimu zinaonyesha kuwa idadi ya watu walioambukizwa virusi vya HIV kupitia kujidunga sindano miongoni mwa waraibu wa dawa za kulevya ilikuwa milioni 1.6 mwaka 2011.

Shirika hilo la kukabiliana na dawa za kulevya la Umoja wa Mataifa UNODC limeanzisha kampeini kote duniani ya kufikisha ujumbe kuwa dawa za kulevya ni tisho kwa jamii na kuwa ni jukumu la kila mmoja kuwalinda vijana dhidi ya dawa hizi hatari huku kauli mbiu ya kampeini hiyo ikiwa acha afya yako iwe kichoche cha maisha yako na si dawa.

Mwandishi:Caro Robi/dpa

Mhariri: Josephat Charo