NIAMEY:Kofi Annan akutana na Rais wa Niger kujadili njaa nchini humo.
24 Agosti 2005Katibu Mkuu wa Umoja wa Matifa,Kofi Annan leo amekuwa na mazungumzo na Rais wa Niger Mamadou Tandja,nchi ambayo imeathiriwa kwa kiasi kikubwa na ukosefu wa chakula.Bwana Annan ameahidi kujenga uhusiano miongoni mwa mashirika ya kutoa misaada,katika jitahada za kupata misaada zaidi na kuepuka matatizo siku za usoni.
Bwana Annan amewaambia waandishi wa habari baada ya mazungumzo yake na Rais Mamadou Tandja,kuwa wamejadili matatizo ya chakula nchini Niger na katika eneo zima la magharibi mwa Afrika na hatua zinazofaa kuchukuliwa kuhakikisha kile kilichotokea mwaka huu,hakipewi nafasi tena kwa siku za usoni.Hata hivyo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema ili yote hayo yafanikiwe kunahitajika ushirikiano na nchi za eneo hilo.
Bwana Annan leo alikuwa katika siku yake ya mwisho ya kutembelea maeneo ya kusini mwa Niger yaliyokumbwa na uhaba wa chakula,ambapo alitembelea pia kliniki na kituo kinachotoa lishe kwa watoto walioathirika na njaa.
Amesema Umoja wa Mataifa unakisia watu zaidi ya milioni 2.5,wapo katika hali mbaya ya ukosefu wa chakula nchini Niger,wakiwemo watoto 32,000 ambao kifo kinawanyemela kutokana na kukosa chakula.