Nicolas Sarkozy jela yamnyemelea
20 Machi 2018Sarkozy alikamatwa mapema leo(20.03.2018) na kuhojiwa na waendesha mashataka wanaohusika na kesi za ufisadi,utakatishaji fedha na ukwepaji kodi nchini humo.
Nicolas Sarkozy mwenye umri wa miaka 63 kutoka chama cha mrengo wa kulia mwenye maneno makali aliyewahi kuiongoza Ufaransa kutoka mwaka 2007 hadi 2012 ni mwanasiasa mwenye ushawishi katika siasa za Ufaransa ambaye amekuwa akiepuka kuguswa katika kesi za kisheria tangu alipoondoka madarakani.
Ni mwanasiasa ambaye ana msimamo mkali juu ya suala la uhamiaji,usalama na utambulisho wa kitaifa na alijaribu kurudi tena katika anga la siasa za kuwania uongozi wakati wa kampeini ya uchaguzi wa rais mwaka jana lakini mwanasiasa huyo ambaye nchini Ufaransa wengi wanamuita 'Sarko'' alidhalilishwa katika uchaguzi wa ndani ya chama chake cha mrengo wa kulia baada ya kuchukua nafasi ya tatu nyuma ya Francois Fillon aliyewahi kuwa waziri mkuu wake. Leo asubuhi kiongozi huyo wa zamani wa Ufaransa alikamatwa na kupelekwa katika ofisi za waendesha mashtaka wanaohusika na masuala ya rushwa katika mji wa Nanterre ulioko nje nje kidogo ya mji wa Paris.
Ikumbukwe kwamba hakuwahi kukubali kuitikia mwito wa kwenda kuhojiwa katika kesi hii hadi wakati huu ikiwa ni mojawapo ya hatua kadhaa za uchunguzi ambazo amekuwa akizikwepa tangu alipoondoka madarakani mwaka 2012 Duru za shirika la habari la AFP zinasema kwamba mwanasiasa mwingine aliyewahi kuwa waziri wa ngazi ya juu katika utawala wa Sarkozy pia nae amehohjiwa leo hii katika sehemu ya uchunguzi huo Sakozy anamulikwa katika uchunguzi ulioanzishwa mwaka 2013 na waendesha mashataka wanaochunguza madai yaliyotolewa mwanzo na aliyekuwa kiongozi wa Libya ambaye ni marehemu kwa sasa Moamer Ghaddafi pamoja na mwanawe wa kiume Seif al Islam kwamba walitowa fedha kufadhili harakati za shughuli ya kampeini ya uchaguzi ya Sarkozy.
Sarkozy adai hana hatia
Madai hayo bila shaka Sarkozy amekuwa akiyakanusha akisema kwamba ni madai yenye nia ya kulipiza kisasi yanayotolewa na wanachama wa utawala wa Libya waliokasirishwa na hatua ya Ufaransa wakati huo ya kushirikia katika hatua iliyoongozwa na jeshi la Marekani ya kuivamia Libya na ambayo ndiyo iliyosababisha kuangushwa kwa utawala wa miaka 41 wa Muammar Gaddafi na hata kuuwawa kwake.
Lakini kesi hii ilimulikwa zaidi mnamo mwezi Novemba 2016 baada ya mfanyabiashara mfaransa mwenye asili ya Lebanon alipokiri kuhusika moja kwa moja kufikisha masanduku matatu yaliyosheheni fedha taslimu kutoka kwa kiongozi wa Libya hadi Ufaransa kama mchango wake wa kusimamia shughuli ya kampeini ya Sarkozy katika duru ya mwanzo ya uchaguzi wa rais.
Ziad Takieddine alipohojiwa kupitia tovuti moja ya masuala ya habari za uchunguzi alisema kwamba aiwahi kufanya safari mara tatu kutoka Tripoli kwenda Paris mwishoni mwa mwaka 2006 na maüpema mwaka 2007 akiwa na masanduku ya fedha kwa ajili ya kampeini ya Sarkozy. Na mara zote hizo anasema sanduku alobeba lilikuwa na kiasi Yuro milioni 1.5 hadi milioni 2 na fedha hizo alikuwa akikabidhiwa na mkuu wa kitengo cha ujasusi katika jeshi la Gaddhafi Abdalla Sennusi.
Washirika wa Sarkozy waandamwa
Aliyekuwa mshirika wa Sarkozy Alexandre Djouhri nae alikamatwa mjini London mwezi Januari mwaka huu na kuachiliwa kwa muda kwa dhamana lakini akarudishwa tena kizuizini mwezi Februari akisubiri kesi,baada ya Ufaransa kutowa warranti wa pili wa kukamatwa kwake kabla ya kesi yake kuanza kusikilizwa Marchi 28.
Djouhri ni mfanyabiashara mwenye umri wa miaka 59 ambaye akifahamika sana miongoni mwa wanachama wakubwa wa chama cha mrengo wa kulia na hata yeye alikuwa akikataa kuitikia mwito wa kwenda kuhojiwa mjini Paris. Nicolas Sarkozy anakabiliwa na kifungo cha hadi mwaka mmoja jela na faini ya yuro 3750 ikiwa atakutwa na hatia ingawa anataka kupata fursa ya kuukatia rufaa uamuzi wa kumfikisha mahakamani akidai kwamba hakufahamu lolote kuhusu udanganyifu uliokuwa ukifanyika .
Mwandishi: Saumu Mwasimba
Mhariri: Mohammed Khelef