Nigeria kulikabidhi eneo la Bakassi kwa Cameroon hii leo
14 Agosti 2008Sherehe ya kubadilishana bendera itakamilisha shughuli ya kulikabidhi eneo la Bakassi linaloshikana na ghuba ya Guinea yenye utajiri mkubwa wa mafuta. Kupeanwa kwa eneo hilo kumeelezwa na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon kuwa mfano wa kuigwa kwa migogoro inayohusiana na mipaka. Msemaji wa rais wa Nigeria amesema kulikabidhi eneo la Bakassi kwa Cameroon ni hatua itakayokuwa na athari zitakazosababisha uchungu mkubwa kwa Nigeria.
Sherehe ya kulikabidhi eneo la Bakassi ambayo imesifiwa na ofisi ya Umoja wa Mataifa katika kanda ya Afrika Magharibi, UNOWA, itafanyika katika mji uliokaribu wa Calabar nchini Nigeria. Mchambuzi wa maswala ya siasa na profesa nchini Cameroon, Aboya Monasse Endong, anaelezea umuhimu wa uamuzi huo.
´´ Naamini uamuzi huo utasaidia kuondoa wasiwasi na hofu katika jamii ya Wanigeria ambao kwa muda mrefu walikuwa wakiamini wanajeshi hawataondoka katika eneo la Bakassi.´´
Vyombo vya habari vya Nigeria vimeripoti kwamba usalama umeimarishwa katika eneo la Bakassi hivyo kuashiria sherehe hiyo huenda ikafanyika katika eneo hilo. Maafisa wa Nigeria hawajasema lolote kuhusu madai hayo ya vyombo vya habari.
Mchakato wa kalikabidhi eneo la Bakassi kwa Cameroon umecheleweshwa kwa miaka miwili na umekumbwa na tofauti za kisiasa, matumizi ya mtutu wa bunduki na kesi kuwashilishwa mahakamani. Afisa wa serikali ya Cameroon amesema hii leo kukamilishwa kwa mchakato wa kulirudisha eneo la Bakassi kwa Cameroon kunamaliza mgogoro ulioanza mnamo mwezi Disemba mwaka 1993 wakati ambapo jeshi la Nigeria lilivikalia na kuvidhibiti vijiji kadhaa katika eneo hilo.
Kwa mara ya kwanza Cameroon iliwasilisha kesi kwa mahakama ya kimataifa ya jinai mjini The Hague nchini Uholanzi mnamo mwezi Machi mwaka wa 1994. Baada ya vita vya kisheria, mahakama hiyo iliamua mnamo mwezi Oktoba mwaka wa 2002 kwamba eneo la Bakaasi linapaswa kurudishwa kwa Cameroon. Uamuzi huo ulifikiwa kwa misingi ya mkataba wa mwaka wa 1913 uliosainiwa kati ya wakoloni wa zamani wa Cameroon, Uingereza na Ujerumani.
Cameroon na Nigeria zilitiliana saini makubaliano yaliyojulikana kama Green Tree mnamo mwezi Juni mwaka wa 2006 huko mjini New York nchini Marekani. Makubaliano hayo yalifikiwa chini ya upatanisho wa Marekani na kushuhudiwa na katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan, hivyo kufungua mlango kwa Nigeria kuondoka kutoka eneo la Bakassi. Lakini hatua ya kulikabidhi eneo hilo kwa Cameroon imehatarishwa na changamoto za kisheria za dakika za mwisho na mashambulio kadhaa hatari ya umwagaji damu.
Mwezi uliopita mahakama ya mjini Abuja nchini Nigeria ilitoa amri ya kisheria kuikataza serikali isilirejeshe eneo la Bakassi kwa Cameroon kulingana na tarehe ya mwisho iliyokuwa imekubaliwa. Licha ya hatua hiyo rais wa Nigeria Umaru Yar´Adua amesisitiza kwamba nchi yake haitazembea wajibu wake wa kimataifa. Msemaji wa rais huyo amesema kulikabidhi eneo la Bakassi kwa Cameroon, licha ya kuwa uamuzi unaosababisha uchungu kwa kila Mnigeria, ni ahadi ambayo Nigeia imeitoa kwa jumuiya ya kimataifa na viongozi wa nchi hiyo wana jukumu la kuitimiza.
Katika miezi ya hivi karibuni, eneo la Bakassi linaloaminiwa kuwa na raslimali ya mafuta na gesi na maeneo ya uvuvi, limekuwa uwanja wa vita kati ya wanajeshi wa Cameroon na makundi ya waasi wenye silaha yanayopinga eneo hilo kuridishwa kuwa himaya ya Cameroon. Takriban watu 50 wameuwawa katika mapigano hayo.