Nigeria na majirani zake watangaza vita dhidi ya Boko Haram
18 Mei 2014Wakikutana mjini Paris, rais wa Nigeria Goodluck Jonathan na wenzake kutoka Benin, Chad, Cameroon na Niger wameidhinisha mpango wa kuchukua hatua kupambana na kundi hilo ambalo linalaumiwa kwa kuhusika na vifo vya watu 2,000 mwaka huu pamoja na kutekwa nyara mwezi uliopita kwa wanafunzi wasichana kutoka kaskazini mashariki ya Nigeria.
Wakisisitiza kitisho chao , Boko Haram wanatuhumiwa kufanya shambulio jingine katika mkesha wa mkutano huo, wakiwauwa wanajeshi wa Cameroon na kuwateka nyara wafanyakazi kumi raia wa China nchini Cameroon.
"Tumeona kile ambacho kundi hili linaweza kukifanya ," Rais wa Ufaransa Francois Hollande amesema.
"Wamewatishia raia, wameshambulia shule na wamewateka nyara raia wa nchi kadha.
"Wakati zaidi ya wasichana 200 wanashikiliwa katika mazingira magumu na kuwa na uwezekano wa kuuzwa katika utumwa, hakuna swali la kuulizwa, ni hatua tu zinazopaswa kuchukuliwa," Hollande ameongeza.
Mkakati wa pamoja
Mpango huo wa kuchukua hatua utajumuisha juhudi za pamoja za upelelezi zenye lengo la kuwapata wasichana hao, kubadilishana taarifa za ujasusi na juhudi za pamoja za kufanya doria katika mpaka wa mataifa ya eneo hilo, kwa mujibu wa majumuisho ya mkutano huo.
Katika hatua za muda mrefu, nchi hizo zimekubaliana kuunda mkakati wa kupambana na ugaidi chini ya tume ya bonde la ziwa Chad ambayo ipo lakini haina makali, kwa kuwa na utaalamu wa kiufundi na msaada wa mafunzo kutoka Uingereza, Ufaransa, Umoja wa Ulaya na Marekani.
Vikwazo dhidi ya Boko Haram
Nchi hizo pia zimekubaliana kuweka vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya viongozi wa Boko Haram pamoja na kundi jingine la Nigeria la Kiislamu la Ansaru.
Afisa mwandamizi wa wizara ya mambo ya kigeni nchini Marekani Wendy Sherman amesema vikwazo hivyo vinaweza kupendekezwa katika baraza la usalama la Umoja wa Mataifa mapema wiki ijayo.
Sherman amesifu majadiliano ya jumamosi kuwa "ni muhimu na yenye maana".
Ameongeza: "Tutaona hatua ambazo zinakuwa bora kila wakati na uratibu."
Uingereza itakuwa mwenyeji wa mkutano ujao mwezi ujao.
Nchi za Afrika magharibi tayari zimeahidiwa msaada katika vifaa vya uchunguzi na ushauri wa kitaalamu wa kijeshi kutoka Uingereza, Ufaransa na Marekani wakati wakijaribu kupambana na kundi ambalo Hollande amesema limeunda mahusiano na makundi ya kigaidi barani Afrika.
Viongozi hao wa Afrika wamesisitiza onyo hilo.
"Tuko hapa kutangaza vita dhidi ya Boko Haram," rais wa Cameroon Paul Biya amesema. Mwenzake wa Benin Thomas Boni Yayi ameongeza: "Kutokuwapo uvumilivu wa kidini hakuna nafasi katika bara la Afrika."
Na Idriss Deby wa Chad ameonya: "Magaidi tayari wamekwisha fanya uharibifu mkubwa. Kuwaachia kuendelea kutasababisha hatari ya kuruhusu eneo lote kutumbukia katika machafuko."
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: Sudi Mnette