Nigeria yawacharaza wenyeji Australia 3-2 Kombe la Dunia
27 Julai 2023Timu ya taifa ya wanawake ya Nigeria imeishushia kichapo Australia ambao pia ni wenyeji wa michuano ya Kombe la Dunia la Wanawake kwa magoli 3-2 katika mchezo uliotamatika muda mfupi uliopita.
Soma zaidi: Timu nne za Afrika zinashiriki Kombe la Dunia la Wanawake 2023
Australia walikuwa wa kwanza kupata goli katika dakika za nyongeza kipindi cha kwanza kupitia kwa Emily Van Egmond kabla ya Uchenna Kanu wa Nigeria kusawazisha katika muda huo huo wa nyongeza kipindi cha kwanza.
Hadi wakati wa mapumziko, timu hizo zilikuwa zimetoshana nguvu, japo dakika ya 65 ya mchezo beki wa Nigeria Osinachi Ohale akaipatia Nigeria goli la pili na dakika saba baadaye Asisat Oshoala akapachika goli la tatu na kuifanya ngome ya Nigeria kujihakikishia alama tatu muhimu katika mchezo huo.
Ushindi huo umefufua matumaini yaliyoanza kupotea kwa timu za Afrika mara baada ya Zambia kutolewa katika michuano hiyo katika hatua ya makundi.
Nigeria sasa inaongoza kundi B kwa alama 4 sawa na Canada walioko nafasi ya pili huku vibonde Jamhuri ya Ireland wakiwa mkiani.
Nigeria itakutana na Jamhuri ya Ireland ambayo tayari imeshafungashwa virago hapo jana katika mchezo wao mwisho na iwapo itashinda, basi itajikatia tiketi ya kuingia katika hatua ya 16 bora ya michuano hiyo ya Kombe la Dunia kwa Wanawake ya 2023.
Canada ambao wako kundi moja na Nigeria watacheza mechi yao ya mwisho dhidi ya Australia na mchezo huo utaamua ni nani atatinga hatua ya 16 bora na nani ataungana na Jamhuri ya Ireland kurejea nyumbani.
Mechi za mwisho za kundi B zitachezwa kwa wakati mmoja na baada ya hapo mbivu na mbichi zitakuwa zimeshajulikana.