Umoja wa Afrika walaani wageni kushambuliwa Afrika Kusini
4 Septemba 2019Rais Muhammadu Buhari amechukua hatua hiyo kufuatia magenge ya raia wa Afrika Kusini kuvamia biashara katika sehemu tofauti za nchi hiyo, wakipora mali na kuchoma magari katika wimbi jipya la chuki dhidi ya wageni. Buhari alimuagiza waziri wake wa mambo ya nje kumuita balozi wa Afrika Kusini ili kuelezea masikitiko yake juu ya vitendo wanavyofanyiwa raia wa Nigeria na kutaka hakikisho la usalama wao pamoja na mali zao.
Serikali ya Nigeria kupitia Ukurasa wake wa Twitter iliandika kwamba ujumbe wake utawasili mjini Pretoria siku ya Alhamis na kukutana na rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa. Rais Ramaphosa amelaani mashambulizi hayo akisema hayakubaliki.
"Mashambulizi dhidi ya wafanyabiashara wa kigeni ni suala lisilokubalika na hatuwezi kuruhusu litokee Afrika Kusini ambako watu wanaondesha biashara zao wanashambuliwa, mali zao kuporwa na kuchomwa moto kitu ambacho ni kinyume na sisi waafrika Kusini tunavyoamini"
Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika Moussa Faki, alilaani ghasia hizo lakini akaongeza kuwa ametiwa moyo na hatua zilizochukuliwa na Afrika Kusini za kuwakamata watuhumiwa.
Nalo shirikisho la mpira wa miguu la Zambia FAZ, limefuta mechi ya kirafiki iliyokuwa ifanyike mjini Lusaka siku ya Jumamosi kutokana na vurugu hizo. Kwenye taarifa yake iliyoitoa Jumanne, FAZ inasema sababu za kusitisha mechi hiyo ni hali ya kiusalama nchini Afrika Kusini, hata kama Zambia ilikuwa mwenyeji.Soma zaidi...
Hadi kufikia sasa watu watano wamepoteza maisha kutokana na ghasia hizo, na polisi wamewakamata zaidi ya watu 80 kuhusiana na matukio hayo ya chuki dhidi ya wageni. Raia kadhaa wa Nigeria walitumia mitandao ya kijamii kuhamasisha watu kuyasusia makampuni ya Afrika Kusini ikiwemo kampuni ya kutoa huduma ya simu ya MTN, DSTV na duka la Shoprite.
Ghasia za chuki dhidi ya wageni Afrika Kusini zina historia ndefu ambapo wazawa wamekuwa wakiwalaumu raia wa kigeni kwa kiwango kikubwa cha ukosefu wa ajira. Afrika Kusini ni kitovu cha wahamiaji wa kiuchumi kutoka nchi jirani za Lesotho, Msumbiji na Zimbabwe. Raia wengine hutoka mbali kama vile Kusini mwa Asia na Nigeria. Mashambulizi dhidi ya maduka ya wageni yalianza siku moja baada ya madereva wa malori kuanza mgomo wa nchi nzima siku ya Jumapili kupinga hatua ya kuwaajiri madereva wa kigeni. Vurugu hizo zimetokea kuelekea kongamano la kiuchumi la dunia litakalofanyika mjini Cape Town kuanzia Jumatano.
Vyanzo: AFP/Reuters