Nigeria yavunja rikodi mbaya ya ulaji rushwa
20 Juni 2005Kulingana na ripoti ya shirika la kimataifa linalopambana na ufisadi kwa jumla na hususan rushwa la Transparency International kuhusu hali ya mambo mwaka jana wa 2004, miongoni mwa nchi 25 zinazokabiliwa na rushwa duniani, 9 ni kutoka bara la Afrika.
Ripoti hiyo ilichapishwa kwa kuzingatia hali katika nchi 146 kutoka pembe nne za dunia.
Kwenye orodha ya nchi ambako rushwa umekithiri barani Afrika, Nigeria inaongoza, ikifuatiwa na Chad. Halafu zinakuja nchi tatu ambazo ziko sawa sawa, ikiwa ni pamoja na Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, Ivory Coast na Angola.
Hata hivyo kuna pia nchi barani Afrika ambazo zinafanya vizuri. Botswana yaongoza, ikifuatiwa na Tunisia.
Na licha ya mkasa wa rushwa uliyomhusisha hivi karibuni makamu rais wa Afrika ya kusini Jacob Zuma na ambao ulipelekea kufukuzwa kazi, Afrika ya kusini imechukuwa nafasi ya tatu ya nchi zisizoathiriwa na rushwa, sawa na visiwa vya Mauritius na Ushelisheli.
Ripoti hiyo ya Transparency International, ilichapishwa kwa kuzingatia taarifa za wafanyabiashara na watalaamu katika nchi hizo.
Ni hivyo basi, kuanzisha kampuni au shirika lako binafsi ni vigumu katika nchi kadhaa, lakini nchini Nigeria, ni taabu sana. Amesema mfanyabiashara Chidi- Martins Opera ambae kalazimika kulipa rushwa mara tatu zaidi ya kiwango cha ushuru wa dola 75 kilichopangwa rasmi.
Alisema, “Unapaswa kutoa hongo kwa maafisa, laa sivyo faili lako haitosonga mbele kukiwa na hatari ya kupotea.
Wakati mungine, unapitia kwa watu wengine wa kati kati ili kupata wateja. Wao pia wanakudai pesa.
Usipotoa, huwezi kufanya biashara nchini Nigeria.
Tunatumika sana, lakini watu wengine ndiwo hunufaika”. Amemalizia kusema mfanyabiashara huyo wa nchini Nigeria.
Hali hiyo inapatikana pia katika nchi kadhaa barani Afrika ambako ulaji mlungula umekwamisha miradi ya maendeleo kwa kuwavunja moyo watu kuunda mashirika ya kibinafsi na kupotosha mali ya umma na kuiweka mikononi mwa watu wachache.
Nigeria ni nchi ya kwanza kuzarisha mafuta mengi barani Afrika na ya 8 duniani, lakini mabilioni ya dola za pato kutokana na mafuta ya petroli ziliporwa na viongozi, na nchi haina la kuonyesha kama nchi inayozarisha mafuta.
Idadi kubwa ya wakaazi wake milioni 140 wanaishi na chini ya dola 1 kwa siku. Hospitali, shule, barabara ni mbovu na umeme na maji hukatika kila mara.
Kwa hiyo rushwa umegeuka kuwa kitendo cha kawaida tu. Waalimu, waganga, hata waandishi habari wanakula wakati polisi wakitafuta pesa kwa kuwakandamiza madreva katika viziwizi vya barabarani.
Pamoja na kuwa kizingiti kwa wafanyabiashara wa taifa, rushwa unawavunja moyo pia wawekezaji wa kigeni.
Katika kujaribu kuboresha hali ya mambo, nchi 24 za Afrika zilisaini kile kilichotajwa mpango wa uokozi, kwa lengo la kuwashawishi wawekezaji wa kigeni, wakati ambapo juhudi zikifanywa kuhakikisha utawala bora.
Mfumo huo ambao unahusika kwa njia moja ama nyingine na uchunguzi, ni katika mpango mzima wa maendeleo kwa ajili ya Afrika NEPAD kwa ufupi.
Hadi sasa lakini hakuna hatua kubwa imeshapigwa katika fani hiyo.
Mfumo huo ulijaribiwa kwa mara ya kwanza nchini Rwanda na Ghana, lakini bila mafanikio kwa sababu maafisa katika nchi hizo hususan nchini Ghana, walichukuwa hatua madhubuti za kuficha dalili zote za ufisadi na ulaji rushwa katika sekta ya wafanyakazi wa serikali.
Kwa sasa, rais wa Afrika ya kusini Thabo Mbeki ametoa mfano mzuri wa kupambana na rushwa kwa kumfukuza makamu wake Jacob Zuma. Kenya ambayo ni miongoni mwa nchi zinazokabiliwa na rushwa imesema inataka kuiga mfano wa Afrika ya kusini.