Nini kilivuruga mazungumzo ya Trump na Kim huko Hanoi?
1 Machi 2019Nani anasema ukweli?
Katika muktadha huu inaonekana kwamba Korea Kaskazini ndio wenye kusema ukweli. Mkutano wa Trump na Kim uliokuwa ukisubiriwa kwa hamu uliofanyika mji mkuu wa Vietnam Hanoi siku ya Jumatano na Alhamis, ulimalizika bila ya viongozi hao kusaini makubaliano yoyote. Trump alizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya mazungumzo yake na Kim, akisema mvutano juu ya vikwazo ulikuwa ndio msingi wa makubaliano.
"Kimsingi walitaka kuondolewa vikwazo kabisa na tusingeweza kufanya hivyo". Ilibidi tuondoke katika hilo", alisema Trump. Masaa machache baadae maafisa wawili waandamizi katika ujumbe wa Korea Kaskazini nao waliwaeleza waandishi wa habari kwamba hicho sicho alichokihitaji Kim. Walisisitiza kwamba Kim aliomba tu sehemu ya vikwazo kuondolewa kama sharti la kufunga eneo kuu la nyuklia la nchi hiyo.
Waziri wa mambo ya nje Ri Yong Ho alisema Korea Kaskazini ilikuwa tayari kuwasilisha kwa maandishi usimamishaji wa kudumu wa nusu ya makombora ya nyukilia na yale ya masafa ya kati. Kaimu waziri wa mambo ya nje Choe Sun Hui alisema namna Trump alivyopokea taarifa hiyo ilimshangaza Kim na kuongeza kwamba huenda kiongozi huyo amepoteza nia ya kuendelea kushughulika na masuala ya nchi hizo mbili.
Kwa mujibu wa afisa wa ngazi ya juu katika wizara ya mambo ya nje ya Marekani ambaye hakutaka jina lake kutajwa alisema "kimsingi Korea Kaskazini walitaka kuondolewa vikwazo vyote". Lakini alikiri kwamba madai ya Korea Kaskazini yalikuwa tu ni kwa Marekani kuunga mkono kuondolewa kwa vikwazo vya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa vilivyowekwa machi 2016 na havikujumuisha maazimio mengine ya muongo mmoja uliopita.
Walichokihitaji Pyongyang alisema kilikuwa ni kuondolewa vikwazo ambavyo vinaathiri uchumi na maisha ya raia kama alivyosema waziri wa mambo ya nje wa Korea Kaskazini.
Vikwazo vya Baraza la Usalama
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa viliweka maazimio kadhaa yanayoilenga Korea Kaskazini na kuifanya kuwa nchi yenye vikwazo vingi ulimwenguni. Kwahiyo Kim ni kama alikuwa akitafuta unafuu wa vikwazo hiyvo, ikiwa ni pamoja na marufuku iliyowekwa katika kila kitu ikiwemo chuma, mali ghafi, vitu vya kifahari, vyakula vya baharini, makaa ya mawe, bidhaa za petroli na hata malighafi ya mafuta hayo.
Lakini Kim hakuwa anatafuta kuondolewa vikwazo katika silaha. Hivyo viliwekwa mapema mwaka 2006 wakati Korea Kaskazini ilipofanya jaribio lake lwa kwanza la Nyuklia. Wakati ikidai kwamba silaha za nyuklia zinahitajika kwa ajili ya ulinzi binafsi, ilikubali kwa muda huu vikwazo vya moja kwa moja vinavyohusiana na silaha hizo sambamba na teknolojia ya makombora. Lakini imekuwa ikichukulia vikwazo katika maeneo mengine kama vile biashara kuwa ni uovu na ilikuwa ikiashiria kuvitumia kama sababu ya majadiliano.
Lakini maafisa wa Marekani wanasema Trump na wazungumzaji wake waliyatupilia mbali madai hayo kwasababu wanadhani kuiondolea vikwazo vya baada ya 2016 vitakuwa ni sawa na mabilioni ya dola ambayo Korea Kaskazini inaweza kuyatumia kuendeleza ufadhili wa mpango wake wa nyuklia na makombora.
Wanasema pia hilo halikuja kwa mshangao, kwasababu taifa hilo limekuwa likishinikiza madai hayo kwa wiki kadhaa katika mazungumzo ya ngazi ya chini. Hata hivyo pande zote zilionekana kudhamiria kutoka na matumaini katika mkutano huo, ambao Trump anasema kwa ujumla ulikuwa rafiki na wenye kuzaa matunda. Vyombo vya habari vya Korea Kaskazini havikugusia uamuzi wa Trump kuondoka mkutano huo bila ya makubaliano na kuashiria kwamba Korea Kaskazini ilitazamia mazungumzo zaidi.
AP