1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nini kitarajiwe Sochi?

22 Novemba 2017

Urusi,Iran,na Uturuki waizungumzia Syria ikiwa ni siku chache baada ya ziara ya rais Assad wa Syria katika mji huohuo wa kitalii

https://p.dw.com/p/2o52q
Russland Sotschi | Rohani & Putin & Erdogan
Picha: Reuters/Turkish Presidential Palace/Kayhan Ozer

Viongozi wa Uturuki na Iran wako katika mji wa kitalii wa Sochi nchini Urusi kwa ajili ya mazungumzo na mwenyeji wao, Rais Vladmir Putin, juu ya ufumbuzi wa kisiasa baada ya kumalizika vita nchini Syria, siku mbili tu baada ya Rais Putin kumkaribisha Rais Bashar Al Assad wa Syria na pia kuzungumza na mwenzake wa Mamerakni, Donald Trump, juu ya kuumaliza mzozo huo.

Mazungumzo ya mjini Sochi yameshaanza huku mwenyeji rais Vladmir Putin kifungua mkutano huo kwa kutowa mwito wa kujitolea na maridhiano kwa pande zote kwa ajili ya kuufikisha mwisho mgogoro wa Syria wa takriban amiaka sita na nusu . Putin amesema ni wazi kwamba mchakato wa mageuzi hautakuwa rahisi na bila shaka utahitaji kuwepo utayarifu wa kujitolea na maridhiano kutoka kila upande husika  na juu ya hilo binasi Putin anasema anayaweka matumaini makubwa kwa Iran na Uturuki katika juhudi zao za kuhakikisha uwezekano wa kufikiwa mafanikio.

Russland Sotschi | Rohani & Putin & Erdogan
Picha: Reuters/Turkish Presidential Palace/Kayhan Ozer

Rais Rouhani kwa upande mwingine anasema ni muhumi kwa kila upande kuchangia kuelekea suluhisho la kisiasa katika mgogoro wa Syria  ambalo litakubalika na wanancho wote wa Syria.Rouhani anasema vikosi vya kigeni katika mgogoro huo wa Syria vinabidi viondoke na kikiso chochote kutoka nje kinaweza tu kuruhusiwa ndani ya nchi hiyo endapo serikali ya Syria itatowa ridhaa hiyo.

Mkutano huo mdogo wa kilele  wa nchi tatu ambazo mwanzoni mwa mwaka huu zilisaidia kusimamia kupatikana makubaliano ya kusitisha vita kati ya vikosi vya serikali ya Syria na na makundi ya wapiganaji wa upinzani nchini humo yanafanyika siku mbili baada ya rais wa Syria Bashar al Assad kumtembelea Putin hukohuko Sochi.Iran na Urusi ni waungaji mkono wakubwa wa rais Assad na utawala wake wakati ambapo Uturuki kwa upande wa pili inaunga mkono wapinzani wa ndani ya Syria.

Ikulu ya Urusi Kremlin ilisema  kabla ya mkutano huo kati ya Assad na Putin kwamba rais huyo wa Urusi aliwahakikisha  viongozi wa Uturuki na Iran kwamba nchi yake  itashirikiana na uongozi wa Syria kuhakikisha kwamba makubaliano yoyote ambayo yanaweza kufikiwa siku hii ya leo Jumatano kati ya Urusi Iran na Uturuki yatakuwa muhimu.

Russland Sotschi Treffen Assad und Putin
Picha: Reuters/Sputnik/M. Klimentyev

Hata hivyo haijawa wazi ikiwa ikulu ya Urusi itaweka shinikizo lolote dhidi ya Assad kukubali makubaliano ya aina yoyote yanayoweza kufikiwa katika mkutano huo wa kilele.Ama kwa upande mwingine mjumbe wa Umoja wa Mataifa kuhusu Syria amesema pia anapanga kuandaa duru mbili za mazungumzo ya amani mjini Geneva mwezi Ujao wa Desemba kati ya serikali ya rais Bashar al Assad na upinzani ambao umeshadhoofika.

Mazungumzo hayo yanapangwa katika wakati ambapo tayari Urusi ambayo ni mshirika wa karibu zaidi wa Serikali ya Syria ikichukua nafasi kubwa zaidi ya kidiplomasia katika juhudi za kumaliza vita hivyo vya takribana miaka sita na nusu.Steffan De Mistura ameweka wazi juu ya dhamira yake hiyo leo Jumatano wakati akizungumza mbele ya mkutano wa makundi makubwa ya upinzani ya Syria unaofanyika huko mjini Riyadh nchini Saudi Arabia.Mjumbe huyo pia ametowa mwito katika mkutano huohuo wa kuwataka wapinzani kushirikiana  kama upinzani katika mazungumzo hayo akisema kwamba Umoja wa Mataifa unataka kuuonesha ulimwengu kupitia Wasyria wenyewe kwamba mazungumzo ndio njia pekee ya kuelekea hatua itakayoamua mustakabali wa Syria.

Mwandishi: Saumu Mwasimba

Mhariri: Mohammed Khelef

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW