Nishati mbadala yagubika mazungumzo Berlin
1 Novemba 2013Matumizi ya nishati mbadala nchini Ujerumani ndio yaliyogubika mazungumzo ya kuunda serikali kuu ya muungano mjini Berlin.Mada kuu ni kuhusu namna ya kupunguza kupanda bei ya nishati wakati Ujerumani inajiandaa kuondokana na nishati ya makaa mawe na kuingia katika enzi za nishati inayotokana na nguvu za upepo na mwangaza wa jua.
Waziri mkuu wa jimbo lenye wakaazi wengi zaidi la Ujerumani-Northrhine Westfalia,bibi Hannelore Kraft wa kutoka chama cha Social Democratic-SPD pamoja na waziri wa nishati wa serikali kuu inayomaliza wadhifa wake Peter Altmeier wa chama cha Christian Democratic Union CDU ndio wanaoongoza mazungumzo ya tume inayaoshughulikia mageuzi katika sekta ya nishati.
Alipoteremka ndani ya gari tu bibi Hannelore Kraft alitambua nini kinamsubiri.Wanaharakati wa shirika la usafi wa mazingira Green Peace wamekusanyika mbele ya wizara ya mazingira katika uwanja wa Postdam na magari matano yaliyojaa makaa mawe na karibu na hapo sampuli za mitambo ya nishati ya upepo."Nishati mbadala badala ya kugharimiwa makaa mawe" ndio ujumbe wa wanaharakati hao kwa waziri mkuu huyo wa jimbo la Northrhine Westfalia.
Sheria ya mageuzi kufanya kazi mwaka 2015
Saa sita nzima walihitaji wajumbe wa tume ya mazungumzo kujadiliana kuhusu nishati mnamo duru hiyo ya kwanza .Magharibi ilipoingia matokeo yakatangazwa:Vyama ndugu vya CDU na CSU vinavyoongozwa na kansela Angela Merkel na kile cha Social Democratic vinataka mswaada wa sheria mpya ya mageuzi ya nishati ifikiwe hadi msimu wa kiangazi mwakani .Bunge la shirikisho Bundestag na baraza la wawakilishi wa majimbo Bundesrat,yakiidhinisha mswaada huo ,sheria ya mageuzi ya nishati ianze kufanya kazi mapema mwaka 2015.
Pande zote mbili zinaonyesha kuridhika na maridhiano yaliyofikiwa katika duru hiyo ya kwanza ya mazungumzo.Waziri mkuu wa jimbo ambalo kijadi ndio shina la migodi ya makaa mawe,bibi Hannelore Kraft amekanusha tuhuma kwamba anayapigania mashirika ya makaa mawe .Waziri wa mazingira Peter Altmaier anayataja mageuzi ya sekta ya nishati kuwa "mradi mkubwa zaidi wa serikali kuu ya muungano."Anasema "Ujerumani inabidi iutanabahishe ulimwengu kwamba nishati mbadala inaweza kupatikana kwa bei nafuu".
Hapo waziri wa nishati alikuwa akijibu hoja kwamba licha ya kuporomoka bei jumla ya umeme,majumbani watu wanalipa bei kubwa kabisa kufidia nishati mbadala.
Kipindi cha mpito kipite salama
Waziri mkuu Hannelore Kraft,anaeshirikiana serikalini na walinzi wa mazingira die Grüne mjini Dusseldorf amekanusha tuhuma kwamba anayapigania mashirika ya makaa mawe."Tunataka kipindi cha mpito kuelekea nishati mbadala kifanyike salama,watu wamudu na kiambatane na usafi wa mazingira" amesema.
Mkuu wa chama cha walinzi wa mazingira Simone Peter aliwaonya CDU/CSU na SPD dhidi ya kile alichokiita kurejea nyuma na kutoa ruzuku kwa migodi isiyokuwa na tija ya makaa ya mawe.
Duru ya pili ya mazungumzo ya tume inayoshughulikia masuala ya nishati itaendelea jumatatu ijayo mjini Berlin.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/dpa/AFP
Mhariri:Yusuf Saumu