Ntaganda afikishwa mahakamani
10 Februari 2014Hata hivyo, kwanza mahakama hiyo ya mjini The Hague itapaswa izithibitishe tuhuma hizo ili kuweza kumfungulia Ntaganda mashtaka. Mchakato huo unaweza kuchukua muda mrefu hadi kukamilishwa. Miezi kadha inaweza kupita kabla ya kesi kuanzishwa.
Mbabe wa kivita huyo anaejulikana kama "mmalizaji" katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo anakabiliwa na tuhuma za uhalifu alioutenda muda mrefu uliopita
Orodha ndefu ya uhalifu
Inadaiwa kwamba kati ya mwaka wa 2002 na 2003 Ntaganda aliekuwa mkuu wa jeshi la kundi la Umoja wa Wazalendo wa Kongo (UPC) alitenda uhalifu mkubwa dhidi ya binadamu. Wakati huo alikuwa chini ya kiongozi wa waasi Thomas Lubanga ambaye tayari ameshahukumiwa.Orodha ya uhalifu alioutenda inajumlisha,uporaji wa mali ,kuwatumia watoto kama askari na ubakaji.
Ajisalimisha kwa Marekani
Tarehe18 Machi 2012, Ntanganda alijisalimisha ghafla kwenye ubalozi wa Marekani nchini Rwanda na kutoka hapo alikabidhiwa kwa ICC. Mahakama hiyo ilikuwa inamsaka tokea mwaka wa 2006 baada ya kuitoa hati ya kimataifa ya kuamuru kukamatwa kwake. Huo ndiyo ulikuwa mwisho wa shughuli za uasi kwa Ntaganda katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambako alijiunga na makundi kadhaa ya waasi.
Mtumishi wa makundi kadhaa ya waasi
Kwa mara ya mwisho, Ntaganda alikuwamo katika kundi la M23 lililoziteka sehemu za jimbo la Kivu ya Kaskazini mnamo mwaka wa 2012. Inadaiwa kuwa Ntaganda alizishika hatamu za uongozi wa kundi hilo kwa kiasi kikubwa. Kwa mujibu wa uchunguzi wa Shirika la kutetea haki za binadamu Human Rights Watch, Ntaganda ndiye aliekuwa mwasisi wa kundi la waasi hao.
Hata hivyo mtaalamu wa masuala ya Kongo kwenye shirika hilo la kutetea haki za binadamu, Ida Sawyer,amesema kuwa aliekuwa anatokea hadharani kama kiongozi wa kundi la M23 alikuwa Sultani Makenga. Mtaalamu huyo ameeleza kwamba lengo la njama hizo lilikuwa kumkinga Ntaganda ili asikamatwe na Mahakama ya Kimataifa ya ICC. Kundi la M23 halikutaka Ntaganda aonekane hadharani kama kiongozi wake .
Mashahidi watakiwa haraka
Watetezi wa haki za binadamu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo siku nyingi walipaaza sauti kutaka Ntaganda apelekwe mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya mjini The Hague.
Mwakilishi wa asasi za kiraia mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Mustafa Mwiti amesema kwake ni wazi kwamba Ntaganda ametenda uhalifu mkubwa,na kwamba anastahili kuhukumiwa adhabu ya juu kabisa.Bwana Mwiti ameiambia DW kwamba Ntaganda hataweza kuepuka adhabu ikiwa aliowafanyia uhalifu watajitokeza na kuutoa ushahidi.
Ukosefu wa ushahidi ni tatizo kubwa
Ukosefu wa mashahidi ni tatizo kubwa sugu kwa Mahakama ya Kimataifa ya mjini The Hague ICC .Mtuhumiwa mwengine wa uhalifu wa kivita nchini Kongo Mathieu Ngudjolo Chui aliachiwa mnamo mwaka wa 2012 kutokana na ukosefu wa ushahidi.
Pia kuhusu shauri la Rais Uhuru Kenyatta Mahakama ya ICC imelalamika kwamba serikali ya Kenya imetatiza sana ukusanyaji wa ushahidi.Kesi ya Rais Kenyatta pia imo hatarini kusambaratika. Hata hivyo mtaalamu wa shirika la kutetea haki za binadamu la HRW Ida Sawyer anatumai kwamba kesi inayomkabili Bosco Ntaganda itafanyika vizuri zaidi. Amesema wahanga wa uhalifu wake watashiriki katika kesi.
Mwandishi: Phillip Sandner
Tafsiri: Mtullya Abdu
Mhariri: Mohammed Khelef