1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nusu ya watoto wahamiaji Warohingya waliachwa mayatima

John Juma Mhariri: Iddi Sessanga
23 Agosti 2018

Utafiti umeonesha kuwa watoto waliodhaniwa kuwa wametenganishwa na wazazi wao kufuatia machafuko ya Myanmar ni mayatima

https://p.dw.com/p/33duc
Rohingya Bangladesch
Picha: DW/A. Marshall

Mwaka mmoja tangu Myanmar ilipoanzisha kampeni dhidi ya jamii ya Warohingya, utafiti umeonesha kuwa watoto waliodhaniwa kuwa wametenganishwa na wazazi wao ni mayatima. Watu 700,000 walikimbia machafuko katika jimbo la Rakhine.

Shirika la kimataifa la misaada kwa watoto Save the Children (STC), limesema leo kuwa nusu ya watoto wa Rohingya waliokimbilia Bangladesh bila wazazi wao kufuatia operesheni ya kijeshi nchini Myanmar, waliachwa mayatima kutokana na machafuko.

Shirika hilo limesema kwa sasa kuna watoto wa Rohingya 6,000 wasiokuwa na wazazi walioko mji wa Cox Bazar, kusini mashariki mwa Bangladesh.

Mkurugenzi mtendaji wa Save the Children nchini Bangladesh Mark Pierce amesema usaidizi wa saa 24 kila siku umekuwa ukiendelea tangu mwaka uliopita huku wafanya kazi wakiwatafuta wazazi wa watoto hao.

Mwaka mmoja baadaye, Pierce amesema ni bayana kuwa kwa wengi, kamwe hakutakuwa na uwezekano wa kuwakutanisha watoto hao na wazazi.

Watoto hao walioachwa yatima walikuwa miongoni mwa Waislamu wengi wa Rohingya waliokimbia kutoka Myanmar jimbo la Rakhine baada ya kukabiliwa na dhuluma kutokana na operesheni kali ya kijeshi, ambayo Umoja wa Mataifa umetaja kuwa takasatakasa au mauaji ya kikabila.

Takriban watoto 370,000 wa Rohingya walikimbilia Bangladesh, baadhi yao wakiwa bila wazazi au walezi
Takriban watoto 370,000 wa Rohingya walikimbilia Bangladesh, baadhi yao wakiwa bila wazazi au waleziPicha: Getty Images/AFP/M. Uz Zaman

Familia kutenganishwa na machafuko

Utafiti huo ambao ni mkubwa zaidi kuwahi kufanywa katika eneo hilo la Cox Bazar, uligundua kuwa asilimia 63 ya watoto walio peke yao, walitenganishwa na wazazi wao au walezi wao, wakati wa vita vya moja kwa moja dhidi ya kijiji chao. Na asilimia 9 ya watu wa familia zao walijaribu kukimbilia Bangladesh.

Shirika la Save the Children halikuwa na habari kuhusu waliko watu wazima katika vijiji au hali zao. Beatriz Ochoa ambaye ni meneja wa uraghibishi katika Save the Children amesema "Tulijua hali ilikuwa mbaya, lakini si kiasi hiki. Hata maafisa wenye uzoefu wa kuwalinda watoto walishangazwa na matokeo ya utafiti huu. Hii itakuwa na maana kubwa katika kazi yetu ”

STC imesema huku japo takwimu zilizotumiwa katika utafiti wao hazikuwa na uwakilishi sawa, watoto walichaguliwa kotekote miongoni mwa idadi ya orodha ya watoto wasiokuwa na wazazi na waliotenganishwa na wazazi na kuongeza kuwa kuna uwezekano mkubwa hali yao inaakisi hali ya watoto wengine ambao hawako pamoja na wazazi wao au walezi.

Picha ya vijiji vilivyoteketezwa moto kaskazini mwa jimbo la Rakhine
Picha ya vijiji vilivyoteketezwa moto kaskazini mwa jimbo la RakhinePicha: Reuters/S. Z. Tun

Misururu ya mashambulizi yaliyofanywa katika kituo cha polisi magharibi mwa jimbo la Rakhine nchini Myanmar, ilisababisha jeshi kuanzisha operesheni kali dhidi ya jamii ya Rohingya mnamo Agosti 25 mwaka uliopita, na kusababisha watu 700,000 kukimbilia Bangladesh, miongoni mwao watoto 370,000.

Machafuko ya Myanmar yamesababisha vifo vya wengi

Watafiti kutoka Australia, Canada na Norway wamekadiria kuwa zaidi ya Warohingya 23,000 wameuawa kufuatia machafuko ya Myanmar.

Wizara ya habari ya Myanmar imelawalaumu wanamgambo wa Rohingya kwa machafuko yaliyotokea Rakhine na kudai watu 400 pekee ndio wamekufa tangu machafuko kuanza, na kwamba walikuwa magaidi wakuu waliouawa katika operesheni ya kijeshi kuwatimua.

Jamii ya Rohingya imekumbwa na mateso kwa muda mrefu nchini Myanmar. Baada ya utawala wa kijeshi kuanza mwaka 1962, hali ya Warohingya iligeuka kuwa mbaya zaidi na kampeni za serikali zilisababisha maelfu ya Warohingya kukimbilia nchi jirani Bangladesh. Sheria mpya ya uraia iliyopitishwa 1982 ilifanya hali kuwa mbaya zaidi- kwani makabila 135 ndiyo yalitambuliwa lakini jamii ya Rohingya haikujumuishwa, na hivyo kuwafanya kuwa watu wasiokuwa na uraia.