1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi wa Marekani.

Mtullya, Abdu Said4 Novemba 2008

Baada ya kampeni ya muda mrefu isiyokuwa na mithili katika historia ya uchaguzi nchini Marekani,watu wa nchi hiyo wanakaribia kutoa uamuzi juu ya nani atakuwa rais wao wa 44.

https://p.dw.com/p/FnF1
Obama apata ushindi wa kwanza.Picha: AP

Baada ya kampeni iliyochukua zaidi za miezi 20, wagombea kiti cha urais nchini Marekani Barack Obama wa chama cha Demokratik amerejea nyumbani katika jimbo la Illinois ,na mshindani wake seneta John McCain pia amerejea nyumbani katika jimbo lake la Arizona ili kufuatilia uchaguzi.

Mjumbe wa chama cha Demokratik Obama mwenye majonzi kutokana na kifo cha bibi yake hapo jana , amepata ushindi wa kwanza katika mji wa Dixville Notch, katika jimbo la New Hampshire. Obama amepata kura 15 na McCain kura sita katika mji huo. Mji huo wenye jadi ya miaka 60 ya kuwa wa kwanza kupiga kura katika uchaguzi umetoa ishara njema kwa mjumbe wa chama cha Demokratik Obama. Watu wa mji huo walipiga kura usiku wa kuamkia leo. Asilimia mia moja ya wapiga kura walishiriki .

Katika mji mwingine-Harts Location Obama amepata kura 17 wakati mshindani wake wa chama cha Republican McCain amepata kura 7.

Katika miaka 40 iliyopita jimbo hilo lilikuwa mnamo mikono ya chama cha Republican.Kwengineko kote nchini Marekani vituo vya kupigia kura vimejaa watu.

Kura za maoni bado zinaendelea kuonyesha kuwa mjumbe wa chama cha Demokratik Barack Obama yupo mbele ya mshindani wake McCain.

Hatahivyo McCain amewaambia watu wanaomuunga mkono wajitayarishe kusherehekea ushindi. McCain aliwaambia watu hao katika mji wa Prescot.Arizona kwamba upepo sasa unavuma katika upande wake.Amesema bado imebakia siku moja kabla ya kuingia Ikulu.McCain amesema atashinda katika uchaguzi huo.

Mshindani wake Obama amesema akiingia Ikulu atamaliza vita vya Irak. Amesema ataiambia serikali ya Irak ichukue jukumu la kulinda watu wake.

Idadi kubwa ya wapiga kura inatarajiwa katika uchaguzi huo. Watu milioni 153 wamejiandikisha kupiga kura-idadi hiyo inawakilisha robo tatu ya wastahiki wote.