1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama ayazungumzia mageuzi ya Myanmar

13 Novemba 2014

Rais wa Marekani Barack Obama amewaambia watawala wa Myanmar kuwa mafanikio ya mageuzi ya kidemokrasia yaliyopatikana nchini humo yameanza tena kurudi nyuma.

https://p.dw.com/p/1DmFT
Myanmar Asean-Gipfel in Naypyidaw Ankunft Barack Obama
Picha: Reuters/K. Lamarque

Lakini Myanmar imeyatetea mageuzi yake ya kisiasa pamoja na namna inavyozishghulikia jamii za walio wachache nchini humo. Hayo ni kabla ya mkutano wa kilele unaoandaliwa leo kati ya Rais wa Myanmar Thein Sein na mwenzake wa Marekani Barack Obama.

Obama anakutana na mwenzake wa Myanmar Thein Sein – jenerali wa zamani aliyegeuka na kuwa mwanamageuzi – pembezoni mwa Mkutano wa Kilele wa Kanda ya Mashariki mwa Asia katika mji mkuu wa Myanmar, Naypyidaw, pamoja na viongozi wengine wa Kusini Mashariki mwa Asia. Kabla ya mkutano huo, Obama alitoa kauli kali kuhusu kasi ya mageuzi kwenye mahojiano na tovuti ya habari ya Myanmar, ya Ireawaddy, yaliyochapishwa kabla ya kuwasili nchini humo jana usiku.

Rais huyo wa Marekani alisema maendeleo hayajapatikana katika kasi ambayo wengi walitarajia wakati mageuzi ya kidemokrasia yalipoanza miaka minne iliyopita. Aliongeza kuwa katika baadhi ya sehemu, kumekuwa na kasi iliyopungua ya mageuzi, na hata kurudisha nyuma hatua zilizopigwa.

Barack Obama und Nina Hachigian ASEAN Gipfel in Myanmar 13.11.2014
Rais Barack Obama akiwa na Balozi wa Marekani katika Jumuiya ya ASEAN Nina HachigianPicha: Getty Images

Ametaja vikwazo vya uhuru wa vyombo vya habari, ukiukaji wa haki za msingi na maovu yanayofanywa katika maeneo ya kikabila nchini humo, zikiwemo ripoti za mauaji ya kiholela, ubakaji na vibarua vya kulazimishwa. Lakini licha ya hayo, Obama amesema Marekani itaendelea kushirikiana kikamilifu na Jumuiya ya ASEAN

Lakini akizungumza kabla ya mkutano huo wa pande mbili, Naibu Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Myanmar U Thant Kyaw amesema nchi nyingi “zinaunga mkono mchakato wao wa mageuzi”.

Amesema, na hapa namnukuu “kama kasi ya mageuzi inapungua, mbona watu wangekuja kuhudhuria mkutano wetu wa kilele? Kwa baadhi ya makundi, mageuzi yetu yanafanyika kwa kasi”. Mwisho wa nukuu. Myanmar ilikuwa chini ya uongozi wa kijeshi kati ya mwaka wa 1962 na 2010, na kutengwa kabisa na baadhi ya nchi za magharibi, lakini vikwazo vingi ilivyowekewa viliondolewa mwaka wa 2012, baada ya Thein Sein kuanza kutekeleza msururu wa mageuzi ya kisiasa na kiuchumi.

Obama hapo kesho Ijumaa ataonyesha ishara ya kumuunga mkono shujaa wa mageuzi ya kidemokrasia nchini Myanmar, na mshindi mwenzake wa Tuzo ya Amani ya Nobel, Aung San Suu Kyi, atakaposafiri ili kukutana naye katika mji wa kibiasharea wa Yangon.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu wa China Li Keqiang amependekeza mkataba wa “urafiki” na nchi za Jumuiya ya Kusini Mashariki mwa Asia – ASEAN, lakini akasisitiza kuwa migogoro ya mipaka katika Bahari ya Kusini mwa China inastahili kutatuliwa moja kwa moja baina ya nchi husika.

China, Taiwan na nchi nne za Jumuiya ya ASEAN zina madai ya ushindani kuhusu mipaka ya baharini ambapo wasiwasi unaendelea kuhusu migogoro hiyo, hata wakati nchi husika zikifanya juu chini kujaribu kufikia makubaliano ya kuitatua.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/Reuters
Mhariri:Yusuf Saumu