1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mpango wa Obama kuhusu gesi chafu wazusha maoni tofauti

4 Agosti 2015

Rais Barack Obama ametoa changamoto kwa Marekani na ulimwengu kuimarisha juhudi za kupambana na ongezeko la joto duniani

https://p.dw.com/p/1G9Jx
Washington Obama Clean Power Plan PK
Rais wa Marekani Barack ObamaPicha: Reuters/J. Ernst

Rais Barack Obama ametoa changamoto kwa Marekani na ulimwengu kuimarisha juhudi za kupambana na ongezeko la joto duniani, wakati akizindua rasmi mpango wa serikali yake wenye utata, unaolenga kupunguza uzalishaji wa gesi ya kaboni kutoka viwanda vya umeme vya Marekani.

Akitangaza mabadiliko ya tabia nchi kuwa kitisho kikubwa kinachoukabili ulimwengu, Obama amesema sheria inayoihitaji sekta ya nishati kupunguza uzalishaji wake wa gesi chafu kwa asilimia 32 kutoka viwango vya mwaka wa 2005 ifikapo mwaka wa 2030 itapunguza malipo ya nishati ya Marekani na kuimarisha afya ya watu walio katika mazingira magumu kote nchini humo.

Mpango huo ambao pia unatoa jukumu la nchi hiyo kuhamia katika nishati mbadala kutoka umeme unaotokana na makaa ya mawe, unalenga kuiwekwa Marekani katika nafasi imara kwenye mazungumzo ya kimataifa mjini Paris baadaye mwaka huu ya kufikia muafaka wa kupambana na ongezeko la joto duniani.

China Kohlekraftwerk in Huaian
Viwanda vya umeme vinavyotumia makaa ya mawe vimepinga mpango wa ObamaPicha: picture-alliance/dpa

Marekani imeahidi kupunguza uzalishaji wake wa gesi chafu kote nchini humo kwa asilimia 26 hadi 28 chini ya viwango vya mwaka wa 2005 ifikapo mwaka wa 2025.

Mpango huo wa Nishati Safi unanuia kuwa sehemu muhimu ya sifa ya rais wa Marekani kuhusu ongezeko la joto duniani, kitu ambacho aliahidi kupambana nacho wakati akiwa mgombea wa urais mwaka wa 2008.

Mtazamo wa viongozi wa Marekani

Waziri wa zamani wa Mambo ya Kigeni wa Marekani Hillary Clinton, anayetafuta tikiti ya chama cha Democratic, amesema atautetea mpango huo, wakati Jeb Bush, mmoja wa Warepublican wanaotafuta kibali cha chama hicho, amesema utawanyima watu nafasi za kazi.

Kiongozi wa upinzani katika Seneti Mitch McConnell amesema sheria hizo mpya zitahujumu viwanda vya nishati na kuongeza gharama za umeme na kuongeza kuwa atakafanya kila awezalo kuupinga.

Spika wa Baraza la Wawakilishi Mrepublican John Boehner ameuita mpango huo kuwa ni “kodi ya nishati”. Amesema anaamini mpango huo wa mwisho ni wa gharama kubwa, na ni matusi kwa Wamarekani wanaojitahidi kujitafutia kipato. Obama amepinga shutuma kuwa mpango wake utaongeza gharama za umeme kwa Wamarekani na kuwaumiza maskini, akisema na namnukuu “ikiwa unajali kuhusu jamii za walio wachache za kipato cha chini, anza kwa kulinda hewa wanayopumua” mwisho wa nukuu. Shirika la Kuhifadhi Mazingira la Marekani limesema jukumu kubwa la nishati safi kama ya jua na upepo litawaridhisha washirika wa Marekani katika mazungumzo ya Paris.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon akisema kuwa ni "mfano wa uongozi wa maono unaohitajika kupunguza uzalishaji wa gesi chafu na kuyakabili mabadiliko ya tabia nchi.

Mwandishi: Bruce Amani/reuters
Mhariri: Josephat Charo