1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama, Ban Ki-moon waitaka dunia iwajibike

Zainab Aziz21 Septemba 2016

Rais Barack Obama wa Marekani na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, wameitolea wito jumuiya ya kimataifa kuongeza juhudi kuishughulikia migogoro duniani kote, hasa mzozo wa Syria na wakimbizi.

https://p.dw.com/p/1K5wS
Rais Barack Obama wa Marekani akihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Rais Barack Obama wa Marekani akihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.Picha: Reuters/K. Lamarque
Viongozi hao wawili walilihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, hii ikiwa ni mara yao ya mwisho kwao kusimama mbele ya baraza hilo kama viongozi.

Katika hotuba yake, Rais Obama, ambaye anamalizia muhula wake wa mwisho mwezi Januari mwakani, ametilia mkazo juu ya mafanikio yaliyopatikana kutokana na utangamano na amewashutumu wale ambao wanajenga kuta na wanaoendelea kujiweka kando na jamii ya kimataifa.

Obama alisema kwamba nchi inayojijengea ukuta ni sawa na kujifungia jela yenyewe, ikiwa ni jibu la wito uliotolewa na mgombea wa urais wa chama cha Repubican nchini Marekani, Donald Trump, anayeishinikiza serikali ya Obama ijenge ukuta katika mpaka wa nchi yake na Mexico.

"Kuongezeka kwa tofauti za kiuchumi kumeibua misimamo mikali ya kidini na kikabila na vile vile kuendeleza utaifa na sera za kujijengea umaarufu," Obama aliiambia hadhara hiyo kuu ya Umoja wa Mataifa.

Mzozo wa wakimbizi

Kuhusu swala la wakimbizi, Rais Obama ametowa wito kwa jamii ya kimataifa kuwa na moyo wa kuwasaidia wakimbizi wa Syria na wa nchi zingine ambao wanatoroka machafuko katika nchi zao.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, akihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, akihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.Picha: Getty Images/AFP/J. Samad
Vile vile, katika mkutano ulioongonzwa na Marekani juu ya wakimbizi, Rais Obama amezisifu Ujerumani na Canada miongoni mwa nchi nyingine ambazo zimefungua milango yake kwa wakimbizi kutoka Syria na nchi nyingine.

Katika hutoba yake, Obama amesema dunia inakabiliwa na mgogoro mkubwa sana. "Zaidi ya watu milioni 65 wamelazimika kuyahama makaazi yao jambo ambalo halijawahi kutokea tangu kumalizika kwa vita kuu ya pili. Miongoni mwao kuna zaidi ya wakimbizi milioni 21ambao wamezikimbia nchi zao, mali zao na yote waliyokuwa wameyazoea."

Kiongozi huyo wa Marekani amesema watu wanakimbia na vifurushi vya nguo migongoni mwao. "Sote tunafahamu kinachotokea nchini Syria si jambo linalokubalika lakini hatuungani pamoja kama tunavyopaswa ili kumaliza mgogoro huu."

Rais Obama amesema nchi yake pia itaongeza idadi ya wakimbizi. jumla wakimbizi laki tatu na elfu sitini watapelekwa katika nchi 50 zilizo ahidi kuwachukua.

Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, ambaye pia anamaliza muhula wake baada ya kuhudumu kwa kipindi cha miaka kumi ametoa hotuba kali kwa kuwasema viongozi wa dunia kwa kushindwa kuishughulikia migogoro ya Syria na Mashariki ya Kati huku akitahadharisha juu ya kuongezeka kwa chuki.

Swala la wakimbizi lililpewa kipaumbele katika Umoja wa Mataifa ambapo nchi wanachama 193 ziliunga mkono azimio la siasa zisizofungamana na upande wowote na pia kuhakikisha njia bora zinatumika katika kushughulikia utitiri wa wakimbizi.

Mwandishi:Zainab Aziz/DPAE
Mhariri: Iddi Ssessanga