Obama kuizuru Afrika, Kenya haimo katika ratiba
21 Mei 2013Ziara hiyo itakayoanza Juni 28 hadi Julai 3 itajumuisha mikutano kati yake na viongozi wa serikali, wafanyabiashara na mashirika ya kiraia, wakiwemo vijana, kwa lengo la kusogeza mbele amani ya kanda na maendeleo. Hii ndiyo itakuwa ziara ndefu zaidi kwa rais huyo ambae kwa kawaida hutumia muda mchache sana katika mataifa mengi anayotembelea.
Msemaji wa Ikulu ya White House Jay Carney, alisema katika taarifa kuwa rais Obama atasistiza umuhimu Marekani inaotilia kwa uhusiano unaozidi kuimarika kati ya nchi hiyo na mataifa ya Afrika kusini mwa Jangwa la Sahara, ikiwemo kupitia upanuzi wa ukuaji wa kiuchumi, uwekezaji na biashara, kuimarisha taasisi za kidemokrasia, na kuwekeza katika vizazi vijavyo vya viongozi wa Afrika.
Mkakati wake mpya wa Afrika
Obama aliwasikitisha waafrika wengi alipotumia masaa machache tu kusini mwa Jangwa la Sahara, katika ziara yake nchini Ghana wakati wa muhula wake wa kwanza. Lakini wakati huu yuko makini kutekeleza mkakati mpya na mpana wa kanda, unaotoa kipaumbele kwa demokrasia na mageuzi ya kiuchumi. Suala linaloulizwa ni iwapo rais huyo mweusi wa kwanza wa Marekani atamtembelea kiongozi wa vita dhidi ya ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini, Mzee Nelson Mandela mwenye umri wa miaka 94 wakati wa ziara hiyo ambapo atambatana na mkewe Michelle.
Lakini uchunguzi wa mapema utajikita pia kwa kiasi kikubwa juu ya mataifa ambayo hayamo katika ratiba ya Obama, ikiwa ni pamoja na Kenya, nchi ya baba yake ambako bado ana ndugu walio hai. Obama mara nyingi hutumia historia yake kujiunganisha na wageni, akikumbuka siku zake za utotoni akiwa nchini Indonesia, urithi wake wa Ireland katika Jamhuri ya Ireland, na vile vile kama mwenyeji wa Hawaii, akijiona kama rais wa kwanza wa Marekani kutoka eneo la Pasifiki.
Matumaini ya kuungana na nchi yake ya asili yafifia
Lakini inaelekea siasa zimezamisha matumaini ya Obama kuungana tena na nchi yake ya asili Kenya. Wadadisi wansema haitaonekana vyema kwa Obama kuonekana na Uhuru Kenyatta, aliechaguliwa kuwan rais wa Kenya mwezi Machi, na ambae atakwenda kujibu mashtaka mwezi Julai, katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu ICC, kwa makosa ya uhalifu dhidi ya ubinaadamu wakati wa vurugu za baada ya uchaguzi mkuu mwaka 2007/2008.
Afisa wa utawala wa Obama aliezungumza kwa sharti la kutotajwa jina, alisema kuchaguliwa kwa Kenyatta lilikuwa jambo lililotia ugumu katika upangaji wa ratiba ya Obama barani Afrika. Obama aliitembelea Kenya mwaka 2006, muda mfupi baada ya kuchaguliwa kuwa Seneta, lakini kabla hajatangaza nia yake ya kuogmbea urais.
Ziara yake barani Afrika itafuatia nyingine kama hiyo iliyofanywa na mke wake Michelle Juni 2011, ambapo alimtembelea Mandela. Obama alikuwa na mkutano mwezi Machi na rais wa Senegal Macky Sall, pamoja na viongozi wa Sierra Leon, Malawi na Cape Verde, akiwasifia kuwa mfano wa maendeleo tunayoshuhudia barani Afrika.
Mwaka 2011,Obama pia aliwapokea viongozi wanne wa Afrika katika ikulu ya White House, wakiwemo marais wa Benin, Guinea, Niger na Cote d'Voire na aliwaahidi kuwa Marekani itaendelea kuwa mshirika muhimu kwa mataifa yanayofuata demokrasia barani Afrika.
Afrika, hadithi ijayo ya mafanikio ya kiuchumi
Mwezi Juni mwaka 2012, Obama alizundua mkakati mpya wa bara la Afrika, ukiwa na lengo la kuimarisha usalama na demokrasia katika bara linalokabiliana na kitisho kutoka kundi la Al-qaeda na mashambulizi ya kiuchumi kutoka China.
Mkakati mpya wa Marekani barani Afrika unalenga kuboresha biashara, kuimarisha amani, usalama na utawala bora na taasisi za kidemokrasia, na kutangaza kuwa bara hili lilioathiriwa na umaskini, rushwa na kutoelewana, linaweza kuwa hadithi ya dunia ya mafanikio ya kiuchumi inayofuata.
Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/afpe,dpa
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman