1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama asema mfumo wa kudumu wa mazingira unahitajika

1 Desemba 2015

Rais Barack Obama wa Marekani amesema dunia inahitaji mfumo wa kudumu kwa ajili ya kushughulikia mabadiliko ya tabia nchi na atahakikisha unapatikana mkataba utakaoimarisha uchumi na kusaidia kulinda mazingira ya dunia.

https://p.dw.com/p/1HFPQ
Rais Barack Obama
Rais Barack ObamaPicha: Reuters/J. Ernst

Akizungumza leo mjini Paris, katika siku ya pili ya mkutano wa kilele wa Umoja wa Mataifa kuhusu mazingira, Rais Obama amesema mkataba imara kuhusu mabadiliko ya tabia nchi utapeleka ishara kwa watafiti na wawekezaji kwamba mabadiliko ni muhimu na hilo litaimarisha uvumbuzi wa nishati.

Amesema anatarajia Marekani itatekeleza majukumu yake ya mazingira kwa ajili ya kuzisaidia nchi nyingine kufikia malengo yao ya nishati. Rais Obama amesema sehemu za mkataba huo wa kimataifa unaojadiliwa mjini Paris zinapaswa kuwa za kisheria.

''Sio tu makubaliano ya kupunguza uchafuzi wa mazingira unaotishia dunia yetu, lakini makubaliano ambayo yatasaidia uchumi wetu kukuwa na watu wetu kustawi bila ya kulaani kizazi kijacho kwa dunia ambayo ni zaidi ya uwezo wake wa kuirekebisha. Sasa hayo yote yatakuwa magumu,'' alisema Rais Obama.

Amesema kuongezeka kwa vina vya bahari na hali ya ujoto kunaweza kudhoofisha rasilimali za kiuchumi na kwamba hayo ni masuala muhimu ya kiuchumi na kiusalama ambayo inabidi yapatiwe ufumbuzi kwa sasa.

Klimakonferenz Paris Gebäude Ausstellung Le Bourget
Picha: Reuters/E.Gaillard

Wakati huo huo, Ufaransa na Ujerumani zimesema zitalipatia bara la Afrika msaada wa mabilioni ya Euro kwa ajili ya kuendeleza nishati mbadala, kabla ya mwaka 2020.

Rais Francois Hollande wa Ufaransa, ametoa tangazo hilo katika mkutano wake na viongozi wa mataifa 12 ya Afrika, waliokusanyika katika mkutano wa kilele wa mazingira mjini Paris, ambapo amesema nchi yake itatoa Euro bilioni 2. Ikulu ya Ufaransa imesema kiwango hicho ni mara mbili ya kile kilichotolewa na nchi hiyo katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Nayo wizara ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo ya Ujerumani, pia imesema itachangia Euro bilioni 3 katika mradi huo. Mwakilishi wa wizara hiyo, Ingrid Hoven amesema leo kuwa kati ya uwezo wa gigawati 10 ambazo Afrika inakusudia kuwa nazo, Ujerumani itasaidia kuchangia gigawati 2. Ujerumani imesema itaongeza mara mbili msaada wake wa mazingira kwa ajili ya nchi zinazoendelea hadi kufikia Euro bilioni 4 kwa mwaka.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE,APE,RTRE
Mhariri: Gakuba Daniel