1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama : Ulaya madhubuti muhimu kwa dunia

Admin.WagnerD25 Aprili 2016

Rais Barack Obama wa Marekani Jumatatu (24.04.2016) amesema Marekani inahitaji kuwa na Ulaya madhubuti ilioungana ili kudumisha utulivu wa kimataifa na kuhimiza kuongeza matumizi ya ulinzi kupamana na Dola la Kiislamu.

https://p.dw.com/p/1IcPG
.
Picha: Reuters/K. Lamarque

Akikamilisha ziara yake nchini Ujerumani ambayo ilikuwa imelenga kuimarisha uhusiano wa kibiashara Obama amewasihi viongozi wa Ulaya kuangalia kupindukia matatizo lukuki yanayayakabili mataifa yao na kudumisha umoja ambao umeleta amani katika bara lao.

Kauli yake hio inakuja baada ya ziara yake aliyofanya awali huko London ambapo aliihimiza Uingereza kuendelea kubakia katika Umoja wa Ulaya wenye nchi wanachama 28 na hiyo kuimarisha juhudi za Waziri Mkuu David Cameron kuepuka kile kinachoitwa "Brexit" yaani kujitowa kwa Uingereza katika umoja huo ambao wanaopinga wanasema kunaweza kuchochea madhara ya kisiasa na kiuchumi kwa nchi hiyo.

Akizungumza wakati akiyatembelea maonyesho ya biashara na viwanda mjini Hannover Jumatatu Obama amesema amekuja kuwakumbusha watu wa Ulaya mafanikio makubwa kabisa waliyoyapata wakiwa kama Umoja wa Ulaya.

Ulaya madhubuti muhimu kwa dunia

"Umoja wa Ulaya ulio madhubuti ni muhimu kwa dunia kwa sababu Ulaya ilioungana inabakia kuwa muhimu kwa ututulivu wetu wa kimataifa. Ulaya inasaidia kudumishwa kwa kanuni na sheria ambazo zinaweza kudumisha amani na kukuza ustawi duniani kote."

Rais Barack Obama wa Marekani akizungujmza Hannover. (25.04.2015)
Rais Barack Obama wa Marekani akizungujmza Hannover. (25.04.2015)Picha: Reuters/K. Lamarque

Obama amesema wasi wasi kuhusiana na kunyakuliwa kwa Crimea kulikofanywa na Urusi na kuzorota kwa ukuaji wa uchumi hususan kusini mwa Ulaya kumepelekea kuzuka kwa mashaka kuhusu kuungana kwa bara hilo na kuchochea siasa haribifu ambazo nazo zimepalilia hofu kuhusu wahamiaji na watu wenye dini tafauti.

Wimbi la wahamiaji wanaokimbia vita nchini Syria limeongeza mvutano katika Umoja wa Ulaya na kuweka shinikizo kwa Kansela Angela Merkel wa Ujerumani ambaye anaonekana kuwa kiongozi mwenye sauti barani Ulaya na ambaye sera yake ya awali ya kufunguwa milango imeathiri msimamo wake wa kisiasa ndani ya nchi.

Ishara kumuunga mkono Merkel

Ziara hiyo ya siku mbili ya Obama nchini Ujerumani inaonekana kuwa ni ishara ya kumuunga mkono kiongozi huyo ambaye wamejenga uhusinao wa karibu kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa Ujerumani mwakani.

Ishara ya mshikamano Obama na Merkel.
Ishara ya mshikamano Obama na Merkel.Picha: picture-alliance/dpa/K. Nietfeld

Ziara hiyo pia imeoyesha kumuunga mkono Merkel na Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameroon kwa dhana pana zaidi ya dhima ya Umoja wa Ulaya kwa dunia.

Obama amesema huu ni wakati muhimu sana na kile kinachotokea katika bara hili kitakuwa na taathira zake kwa watu duniani kote.

Marekani kuweka wanajeshi 250 Syria

Rais Obama pia ametangaza uwekaji wa wanajeshi wa Marekani 250 nchini Syria wengi wakiwa katika kikosi cha operesheni maalum.

Mkutano mdogo wa kilele mjini Hannover . 25.04.2016.
Mkutano mdogo wa kilele mjini Hannover . 25.04.2016.Picha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Jioni hii Obama anaungana na Merkel kwa mazungumzo juu ya masuala yanayoikabili dunia hivi sasa ambayo pia yatahudhuriwa na Rais Francois Hollande wa Ufaransa, Waziri Mkuu wa Italia Matteo Renzi na Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron.

Mazungumzo hayo ambayo yanatajwa kwa mkutano mdogo wa kilele pia yatagusia mapambano dhidi ya wapiganaji wa Dola la Kiislam nchini Syria na Iraq,mzozo wa wakimbizi barani Ulaya ,mzozo wa Libya, kura ya maoni ya Uingereza juu ya uwanachama wake wa Umoja wa Ulaya na makubaliano ya biashara kati ya Marekani na Ulaya yanayopendekezwa pamoja na hatua za kudhibiti mabavu ya Urusi.

Mwandishi : Mohamed Dahman /dpa

Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman