1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Onyo la Baraza la Waandishi wa Habari kwa wanasiasa wa Kenya

Wakio Mbogho7 Septemba 2021

Baraza la Waandishi wa Habari nchini Kenya limewaonya wanasiasa na viongozi wa kitaifa dhidi ya mashambulizi yanayoelekezewa vyombo vya habari nchini humo.

https://p.dw.com/p/401Zn
Kenia Medien Presse Zeitungsleser in Nairobi
Picha: picture-alliance/dpa

Kupitia taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari, Baraza hilo Waandishi wa Habari nchini Kenya limeelezea wasiwasi kufuatia tukio ambapo mwanasiasa mmoja alikishambulia chombo cha habari, na kuwarai wafuasi wake kususia kufuatilia matangazo yake. Kiongozi huyo aliendelea kukidhalalisha chombo hicho cha habari kwa kukiita ‘Githeri media' na ‘Gutter press' ambayo ni majina yanayohusishwa na mashirika yasiyo na maadili. 

Tukio hili ni mojawapo wa matukio ya mashambulizi dhidi ya vyombo vya habari ambayo yamekuwa yakitolea na wanasiasa wanapotofautiana na baadhi ya taarifa zinazorushwa msimu huu wa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022, taifa linaposhuhudia joto la kisiasa. Baraza la waandishi wa habari nchini linasema mwenendo huu ni uchochezi kwa umma, ukiukaji wa haki ya uandishi wa habari na pigo kwa taaluma hiyo kwa ujumla.

''Tutakuwa na majadiliano ya kina''

Jopo kazi la watu 13 lililozinduliwa na Baraza hilo, ambalo linawajumuisha waandishi wa habari, wahariri na wakufunzi, lina siku 22 kutekeleza jukumu la kutathmini hali ya utangazaji wakati huu uchaguzi mkuu unapokaribia. David Omwoyo, ni Afisa msimamizi wa baraza la waandishi wa habari nchini Kenya.

"Tutakuwa na majadiliano ya kina. Maswala ya sheria za utangazaji msimu huu wa uchaguzi tutayaachia jopo hili, litakalowahusisha wadau kwenye sekta tofauti na hatimaye kutupa mwelekeo.” alisema Omwoyo.

Omwoyo anaeleza kwamba endapo kiongozi au mwanasiasa yeyote hajaridhishwa na matangazo ya chombo cha habari au mwandishi wa habari anashauriwa kuwasilisha malalamishi yake kwa kitengo cha malalamishi cha baraza hilo.

Siasa za mitandao ya kijamii

Wanasiasa na umma humetumia mitandao ya kijamii kunadi sera zao
Wanasiasa na umma humetumia mitandao ya kijamii kunadi sera zaoPicha: AFP/T. Karumba

Viongozi wa kisiasa pamoja na umma wameonekana wakitupiana cheche za matusi kwenye mitandao ya kijamii, kila mmoja akivutia kwake. Wiki iliyopita Tume ya Uwiano na Utangamano nchini, NCIC, ilitangaza kwamba imeanzisha kitengo kitakachofuatilia na kushughulikia matamshi ya chuki kwenye mitandao ya kijamii. Wambui Nyutu, naibu mwenyekiti wa tume hiyo, amesema mwenendo umebadilika na sasa mitandao ya kijamii inatumika kueneza chuki na wala sio mikutano ya umma.

"Tuna wasiwasi sana kuambatana na namna mitandao ya kijamii inatumiwa vibaya. Tunanunua vifaa vitakavyotuwezesha kuwakamata watu wanaotumia akaunti gushi za mitandao hii wakifikiri hatutawakamata. Tunafanya kazi kwa karibu na kitengo cha upelelez nchini.” alisema Wambui

Baraza la waandishi wa habari nchini limemtaka mwanasiasa aliyekishambulia chocho cha habari cha CITIZEN TV, kuyaondoa matamshi yake ya kuomba msamaha rasmi.