OPCW: Sumu ya Novichok yakutwa kwenye sampuli za Navalny
7 Oktoba 2020Msemaji wa Kansela Angela Merkel, Steffen Seibert amesema shirika hilo lilifanya uchunguzi wake na limekubaliana na matokeo ambayo tayari yalitolewa katika maabara za Ujerumani, Sweden na Ufaransa.
Soma zaidi: Ujerumani yasema Navalny alipewa sumu ya Novichok
Navalny mkosoaji mkubwa wa Rais wa Urusi, Vladmir Putin alipelekwa Ujerumani siku mbili baada ya kuugua Agosti 20 wakati akiwa safarini kwenye ndege nchini Urusi.
Duru za OPCW zimeeleza kwamba sampuli za damu na mkojo zimeonesha kuwa na kemikali ya ''cholinesterase inhibitor'' ambayo ni sawa na sumu ya Novichok inayoathiri mishipa ya fahamu, iliyopigwa marufuku mwaka 2019. Seibert amesema uchunguzi huo unathibitisha kwa mara nyingine tena kwamba Navalny alikuwa mwathirika wa shambulizi la kemikali ya Novichok. Amesema Ujerumani inarudia wito wake kwa Urusi kuchunguza kikamilifu na kueleza kile kilichotokea kwa Navalny.
Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Fernando Arias amesema matokeo hayo yanatia wasiwasi mkubwa na kwamba matumizi ya silaha za kemikali kwa mtu yeyote ni kinyume na kanuni za sheria zilizoanzishwa na jumuia ya kimataifa.
Suala la kimataifa
Aidha, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Heiko Maas amesema matokeo ya uchunguzi wa shirika la OPCW yatawasilishwa kwa nchi zote 193 wanachama. Amesema jambo hilo ni muhimu kwa sababu sio tu la pande mbili kati ya Ujerumani na Urusi, bali ni suala la kimataifa.
''Hatua zinazofuata sasa zitajadiliwa na washirika wetu, ndani ya Baraza Kuu la OPCW pamoja na Umoja wa Ulaya. Ni wazi kabisa kwamba matumizi yoyote ya silaha za kemikali hayakubaliki na suala hili lazima lijibiwe,'' alifafanua Maas.
Hata hivyo, Urusi imekanusha madai kwamba Navalny alipewa sumu na imesisitiza kwamba vipimo vya madaktari wa nchi hiyo havikupata aina yoyote ya kemikali ya Novichok kwenye mfumo wake wa damu. Urusi imeukosoa uchunguzi wa OPCW ikisema ni ''njama iliyopangwa mapema'' na kwamba wanahitaji kuiona ripoti hiyo. Urusi imesema hivi karibuni itawasilisha matukio yaliyojificha ya wahusika wakuu wa jambo hilo.
Hatua kali zichukuliwe
Wakati huo huo, Navalny ameutaka Umoja wa Ulaya na serikali ya Ujerumani kuchukua hatua kali dhidi ya wanasiasa wachache wenye mamlaka na wafanyabiashara wakubwa walioko karibu na Ikulu ya Urusi na kuwawekea vikwazo.
Katika mahojiano yake na gazeti la Ujerumani, Bild yaliyochapishwa Jumatano, Navalny amemshutumu kansela wa zamani wa Ujerumani, Gerhard Schroeder kwa kuwalinda wauaji na kukubali pesa kutoka kwa Rais Putin. Navalny pia ametoa wito wa kusitishwa kwa ujenzi wa mradi wa bomba la gesi unaogharamiwa na Urusi na Ujerumani unaojulikana kama Nord Stream 2.
(AP, DPA, AFP, Reuters)