Operesheni ya kuifunga kambi ya Calais yaanza Ufaransa
24 Oktoba 2016Ufaransa imeanza kuwaondoa wahamiaji waliopo katika kambi ya Calais kwa lengo la kuifunga kambi hiyo ya porini. Shughuli hiyo inafanywa huku polisi waliojihami wakishika doria. Usiku wa kuamkia leo kulikuwa na makabiliano kati ya polisi na baadhi ya makundi madogo ya wahamiaji walipoteketeza vyoo wakipinga mpango wa kambi hiyo kufungwa.
Mabasi ya kwanza yaliyowabeba wahamiaji kuwaondoa katika kambi ya Calais yalianza safari mapema leo, muda mfupi tu baada ya maafisa wa uhamiaji kuanzisha operesheni hiyo. Mamia ya wahamiaji walionekana wakipiga foleni wakibeba mabegi yao ili kufanyiwa ukaguzi tayari kuhamishwa hadi katika vituo vingine 450 nchini Ufaransa.
Inatarajiwa kuwa kufikia mwisho wa leo, jumla ya wahamiaji 2,500 watakuwa wamehamishwa kutumia mabasi 60 yanayotarajiwa kuwabeba leo. Fabienne Bucco ni meya katika eneo hilo na anasema "Inaendelea salama, tulijua asubuhi hii kutakuwa na watu wengi, na ndiyo inayofanyika, kulikuwa na mamia ya wahamiaji wakisubiri banda kufunguliwa. Tulifungua saa tuliyopanga, kila kitu kikafanyika kiutulivu, hakukuwa na msukumano, watoto walifika taratibu. Tulikuwa na wasiwasi haswa kwa watoto, tukawapa kipaumbele, lakini kila kitu kimeenda shwari".
Serikali ya Ufaransa inasema inafunga kambi hiyo inayowahifadhi watu 6,500, waliotoroka vita na umaskini katika nchi zao, kwa misingi ya kibinadamu. Ufaransa inatarajia kumaliza kuwahamisha wahamiaji hao wote kufikia mwisho wa wiki hii, kisha wiki kesho, ianze kuibomoa na kuifunga kabisa kambi hiyo.
Japo utulivu umeshuhudiwa operesheni ilipong'oa nanga, maafisa wanaotoa misaada wanahofia huenda mamia ya wahamiaji wengine watakataa kuondoka, hivyo kuonya kuwa huenda kukatokea vurugu baadaye shughuli ya kuibomoa kambi itakapoanza.
Lakini hata operesheni ya kuwahamisha inapoendelea, hatima ya watoto-wahamiaji 1,300 ambao wako kivyao kwa kuwa hawakuandamana na wazazi wao haijulikani bayana. Siku ya Ijumaa wiki jana, waziri wa usalama wa ndani ya Ufaransa alisema mazungumzo yanaendelea kuhusu nani anapaswa kuwachukua watoto hao wasiokuwa na uhusiano na wazazi nchini Uingereza.
Ni watoto sabini tu wamehamishiwa Uingereza kuanzia mwanzoni mwa mwaka huu na mapema mwezi wa Oktoba kabla ya kuanza kutekelezwa kikamilifu kwa mpango wa kuibomoa kambi hiyo. Uingereza imekuwa ikishutumiwa kwa kuburuza miguu katika mchakato huo lakini Ufaransa nayo pia inakoselewa kwa kuukwamisha mchakato huo kwa kushindwa kuwasilisha kesi za kutosha za kuzingatiwa.
Mashirika ya hisani ya Uingereza na wabunge wamemwandikia waziri wa mambo ya ndani wa Ufaransa Benard Cazeneuve kufafanuwa kile wanachosema "wasi wasi mkubwa kuhusiana na usalama na hali ya watoto wasioandamana na wazazi wao na watu wazima wanyonge au wasiojiweza.
Mashirika hayo yakiwemo shirika lisilo la kiserikali la Kuwaokowa Watoto la Save the Children ,Baraza la Wakimbizi na Kamati ya Kimataifa ya Uokozi ya Msalaba Mwekundu nchini Uingereza yameandika kwamba "rasilmali zinazotumika hivi sasa hazitoshi kuhakikisha ulinzi wa uhakika kwa watu walioko hatarini kabisa hususan watoto wasioandamana na familia zao".
Barua yao imeonya kwamba kuvunjwa kwa kambi bila ya mandalizi makini kutawaweka katika mazingira ya hatari zaidi wale ambao tayari wako hatarini.
Operesheni ya kuwahamisha wahamiaji hao inafanywa chini ya ulinzi wa maafisa wa polisi waliojihami. Usiku wa jana, baadhi ya wahamiaji waliteketeza moto vyoo katika kambi hiyo na kuwarushia polisi mawe kama njia ya kupinga mpango wa kuondolewa kwao.
Wengi wa wahamiaji na wakimbizi hao waliotoka nchi za Afghanistan, Syria na Eritrea, wamekuwa wakitaka kufika Uingereza, lakini bila mafanikio kufuatia sheria za Umoja wa Ulaya zinazotaka kuwa kwanza watafute hifadhi katika nchi ya Ulaya waliyotangulia kufika.
Mwandishi: John Juma/RTRE/DPE
Mhariri:Iddi Ssessanga