OSCE yataka kuwezesha mazungumzo ya Belarus
28 Agosti 2020Waziri Mkuu wa Albania, Edi Rama ambaye kwa sasa ndiye mwenyekiti wa OSCE ametoa pendekezo la kuizuru Belarus kutokana na mzozo uliosababishwa na matokeo ya uchaguzi wa Agosti 9 yaliyompa ushindi Lukashenko, ambao upinzani umesema uligubikwa na udanganyifu. Ushindi huo wa Lukashenko ulisababisha maandamano makubwa ya nchi nzima.
Akizungumza leo katika mkutano maalum wa Baraza la Kudumu la OSCE kuujadili mzozo wa Belarus na kuzishirikisha nchi zote 57 wanachama wa shirika hilo, Rama amesema wanaamini watapata jibu zuri kutoka kwa serikali ya Belarus.
"Kwa hivyo ninawatolea wito leo viongozi wa Belarus: tafadhali likubalini hili pendekezo. Itumieni hii fursa kwa Belarus kujiepusha na mizozano na kuelekea katika njia ya kufanya mazungumzo na maridhiano," alisisitiza Rama.
Rama amesema lazima pawe na mazungumzo kati ya serikali na upinzani na suala hilo linapaswa kufanyika haraka iwezekanavyo kwa maslahi ya kila mmoja.
Wiki iliyopita Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel alisema kuwa OSCE inaweza kuchukua jukumu muhimu nchini Belarus, lakini Rama amesema shirika hilo halitafuti kuwa mpatanishi, bali tu kuwezesha mazungumzo kufanyika ili kuisaidia Belarus isitumbukie katika mzozo mkubwa.
Belarus yakubaliana na Urusi kuunganisha majeshi
Hayo yanajiri wakati ambapo Lukashenko amesema amekubaliana na Rais wa Urusi, Vladmir Putin kwamba nchi zao zinaweza kuyaunganisha majeshi yao iwapo itapata kitisho kutoka nchi za Magharibi. Mapema leo asubuhi, Lukashenko aliamuru nusu ya majeshi yake kujiandaa kupambana katika kile alichokiita kujibu kitisho kutoka nchini za Magharibi.
Aidha, Kansela Merkel leo ameyaonya mataifa ya kigeni yenye nguvu kutoingilia kati mzozo wa Belarus. Kauli hiyo ameitoa baada ya Rais Putin kusema serikali yake imetenga wanajeshi wa ziada kwa ajili ya kumsaidia Rais Lukashenko. Merkel amesema ana matumaini kuwa jeshi hilo halitapelekwa Belarus.
Hata hivyo, Lukashenko amesema kuwa nchi yake italipiza kisasi iwapo itawekewa vikwazo vyovyote vile na ametishia kuzuia njia za usafirishaji kupitia nchi hiyo na kuzisusia bandari za Lithuania.
Soma zaidi: Lukashenko akabiliwa na changamoto kali
Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa UIaya Josep Borrell ameisihi Urusi kutoingilia kati Belarus. Matamshi hayo ameyatoa leo baada ya kufanya mazungumzo na mawaziri wa mambo ya nje wa umoja huo uliofanyika mjini Berlin, Ujerumani.
Wakati huo huo, shirika la kutetea haki za binaadamu nchini Belarus, Viasna limesema zaidi ya waandamanaji 260 wamekamatwa katika maandamano yaliyofanyika katikati ya Minsk hapo jana. Aidha, takriban waandishi habari 50 wamekamatwa, wakati wakiripoti kuhusu maandamano hayo.
(AFP, DPA, AP, Reuters)