1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Oxfam: Pengo kati ya matajiri na masikini laongezeka

16 Januari 2017

Pengo kati ya matajiri na maskini limeelezwa kuwa kubwa kuliko ilivyodhaniwa awali huku watu wanane tu kuanzia Bill Gates hadi Michael Bloomberg wakimiliki utajiri sawa na wa watu bilioni 3.6.

https://p.dw.com/p/2VqvI
Hunger im Sahel Bildergalerie Tschad
Picha: Andy Hall/Oxfam

Likitangaza matokeo ya uchunguzi wake kuelekea mkutano wa kila mwaka wa viongozi wa kisiasa na kibiashara kutoka kote uliwenguni unaofanyika katika eneo la mapumziko la Davos nchini Uswisi, shirika la kukabiliana na umaskini la Oxfam lilisema kuwa pengo kati ya watu matajiri zaidi na maskini ni kubwa zaidi kuliko ilivyokuwa mwaka mmoja uliopita. Ripoti hiyo iliwahimiza viongozi kufanya mengi zaidi kuliko maneno matupu.
Ripoti hiyo imeonya kuwa iwapo hali hiyo haitasawazishwa, ghadhabu ya umma kutokana na hali hiyo zitaendelea kupanda na kusababisha mabadiliko ya kushtua ya kisiasa kama vile kuchaguliwa kwa Donald Trump kuwa rais wa Marekani na kura ya kujiondoa kwa Uingereza katika Umoja wa Ulaya.

Hali ya kutokuwa na usawa yatishia kuzuka kwa matatizo

Kulingana na mkurugenzi mtendaji wa shirika la Oxfam, Winnie Byanyima, ambaye atahudhuria mkutano huo wa Davos, ni hali ya kutatiza kwa utajiri mkubwa kuwa mikononi mwa watu wachache wakati ambapo mtu mmoja kati ya watu 10 wanaishi kwa dola mbili kwa siku. 
Aliongeza kuwa hali ya kutokuwa na usawa inawakwamisha watu wengi katika umaskini, kuharibu jamii na kudhoofisha demokrasia.
Ripoti kama hiyo mwaka mmoja uliopita ilisema kuwa watu 62 ulimwenguni wanamiliki utajiri sawa na watu wa tabaka la chini ambao ni nusu ya wakaazi wote duniani. Hata hivyo shirika hilo la Oxfam limekadiria upya idadi hiyo kufikia watu wanane kutokana na habari mpya zilizokusanywa na kitengo cha mikopo cha benki ya Uswisi.Shirika hilo la Oxfam lilitumia orodha ya mabilionea ya shirika la Forbes iliyochapishwa mwezi Machi mwaka 2016 kutoa madai yake.
Kulingana na orodha hiyo ya Forbes, Bill Gates ndiye mtu mwenye utajiri mkubwa zaidi akikadiriwa kuwa na utajiri unaofikia dola bilioni 75. Wengine katika orodha hiyo ni Amancio Ortega, mwanzilishi wa jumba la mitindo la Inditex nchini Uhispania, bepari Warren Buffet, mfanyabiashara kutoka Mexico, Carlos Slim Helu, mkuu wa shirika la Amazon Jeff Bezos, mwanzilishi wa mtandao wa Facebook Mark Zuckerberg, mmiliki wa kampuni ya Oracle Larry Ellison na aliyekuwa meya wa New York Michael Bloomberg.
Shirika la Oxfam liliorodhesha mikakati ambayo lilisema lina matumaini ikitekelezwa itasaidia kupunguza hali hiyo ya kutokuwa na usawa.

USA Microsoft Gründer Bill Gates
Bill Gates anayetajwa kuwa mtu mwenye utajiri mkubwa zaidi dunianiPicha: Reuters/B. McDermid

Baadhi ya mikakati iliyoorodheshwa

Baadhi ya mikakati hiyo ni kuhakikisha ushuru wa juu kwa mali na mapato kuhakikisha kuweko kwa usawa na pia kufadhili uwekezaji katika huduma za umma na ajira, ushirikiano bora miongoni mwa serikali katika kuhakikisha wafanyikazi wanalipwa vizuri na kwamba matajiri hawakiuki kulipa ushuru pamoja na viongozi wa kibiashara kujitolea kulipa ushuru na kuwalipa wafanyikazi wao katika viwango bora.
Max Lawson, mshauri wa sera katika shirika la Oxfam, aliwahimiza mabilionea kufanya lililo sawa na kufanya kile ambacho Bill Gates amewataka wafanye ambacho ni kulipa ushuru.
Kulingana na rais na mkurugenzi mkuu wa shirika hilo, biashara huenda zikawa usaidizi mkubwa wa kuimarisha uaminifu. Kampuni zinahitaji kuwa na uwazi kwa wafanyakazi wake kuhusiana na mabadiliko yanayofanyika mahala pa kazi, kuimarisha utendaji kazi na kulipa viwango bora vya mishahara.

Mwandishi: Tatu Karema/ APE/DPAE
Mhariri: Iddi Ssessanga