Pakistan yaiamuru jumuiya ya NATO iondoke kambini
27 Novemba 2011Pakistan imesitisha ushirikiano wake na Marekani pamoja na jumuiya ya kujihami ya NATO. Uamuzi huo unafuatia shambulio la angani katika mpaka kati ya Pakistan na Afghanistan. Ofisi ya waziri mkuu Yousuf Raza Gilani imesema baada ya kufanyika kikao maalumu kati ya maafisa wa serikali na jeshi, kuwa shughuli zote za kidiplomasia, kisiasa, kijeshi na kijasusi zinatakiwa kuchunguzwa.
Wanajeshi hadi 24 wa Pakistan waliuawa kwenye shambulio la angani la jana asubuhi lililofanywa na jumuiya ya NATO. Kwa mujibu wa wanajeshi walionusurika, wengi wa wale waliouawa walikuwa wamelala. Pakistan imezifunga njia zinazotumiwa na jumuiya ya NATO kupeleka mahitaji nchini Afghansitan. NATO na Marekani zimesikitishwa na vifo vya wanajeshi hao na zimeahidi kusaidia katika uchunguzi na kutoa maelezo.
Mwandishi: Josephat Charo
Mhariri: Prema Martin