Pakistan yamuahidi Rice itachukua hatua kali dhidi ya Ugaidi.
4 Desemba 2008Pakistan leo imemuahidi Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Condoleezza Rice kwamba itachukua"hatua kali" dhidi ya mtu yeyote katika ardhi yake atakayegundulikana kuwa alihusika katika mashambulio aya hivi karibuni katika mji wa India wa Mumbai. Bibi Rice alipewa hakikisho hilo na Rais Asif Zardari wakati wa mazungumzo yao mjini Islamabad.
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Condoleezza Rice aliwasili Islamabad akitokea India alikokuweko hapo jana, katika jitihada za kuondoa hali ya mvutano iliotanda akatika eneo hilo, kutokana na hujuma za wiki iliopita katika mji wa Mumbai ambapo India imedai zilifanywa na watu kutoka Pakistan.
Watu 172 waliuwawa katika hujuma hizo. Akizungumza baada ya mkutano wake na Bibi Rice, Rais Zardari alirejea tena ahadi yake kwamba Pakistan iko tayari kusaidia katika uchunguzi juu ya mauaji ya Mumbai , akisema kwamaba serikali haitosaidi tu katika uchunguzi kuhakikisha kwamba ardhi yake haitumiwi kwa kitendo chochote cha ugaidi.
Mchango wa Pakistan katika vita dhidi ya ugaidi ni jambo linalotazamwa upya , ikiwa ni tangu hujuma ya Mumbai, wakati wanaharakati waliokaua na bunduki na mabomu ya kutupa kwa mkono walipozizingira hoteli na maeneo mengine mjini humo kwa muda wa masaa 60.
Akizungumza na waandishi habari baada ya mkutano wake na Waziri mkuu Yousuf Raza Gilani na maafisa wa kijeshi wa ngazi ya juu, waziri Rice alisema anaona kuwa uongozi wa Pakistan umejizatiti kuchukua hatua, na anamatumaini viongozi wa India na Pakistan wataziweka wazi njia za mawasiliano.
Alisema ,"natumai wataziweka wazi njia za mawasiliano. Ni wakati mgumu lakini ieleweke kwamba tunaanzia katika wakati ambapo uhusiano baina ya India na Pakistan umeboreka mno na hilo ni jambo jema. Ni vizuri tuanzie na hali ambapo uhusiano ulikua bora kuliko kuwa katika hali mbaya."
Aidha akiulizwa vipi ,serikali za India na Pakistan zitaweza kushirikiana kwa mafanikio, Waziri huyo wa mambo ya nchi za nje wa Marekani alisema ," kila mtu anataka kuzuwia mashambulio zaidi na nina matumaini ."
Ziara ya Bibi Rice katika eneo hilo imekuja katika wakati ambao India imesema imeviweka viwanja vyote vikuu vya ndege katika hali ya hatadhari,ikionya juu ya uwezekano wa mashambulio kwa kutumia utekeji nyara ndege.
India na Pakistan zimepigana vita mara tatu tangu huru wao kutoka kwa Uingereza 1947 na zote zina silaha za kinuklea. Matukio kama ya hivi majuzi, yanatishia kuzidi kuuzorotesha utaratibu wa amani baina ya nchi hizo na kuzidisha hali ya kutoaminiana.