1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pakistan yaomboleza vifo vya wahanga wa mashambulizi

29 Oktoba 2009

Pakistan ya Kaskazini-Magharibi imetumbukia katika hali ya huzuni baada ya hadi watu 105 kuuawa siku ya Jumatano katika mashambulizi mabaya kabisa ya kigaidi kupata kufanya nchini humo.

https://p.dw.com/p/KINj
Secretary of State Hillary Rodham Clinton speaks about piracy and Somalia, Wednesday, April 15, 2009, at the State Department in Washington. (AP Photo/Manuel Balce Ceneta)
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani,Hillary Clinton.Picha: AP

Mashambulizi hayo yametokea wakati ambapo waziri wa mambo ya nje wa Marekani Hillary Clinton anafanya ziara yake ya kwanza nchini Pakistan.

Umwagaji huo mkubwa wa damu umetokea Peshawar,huku mashambulizi ya kigaidi yakishika kasi nchini Pakistan. Wengi waliouawa katika shambulizi la hiyo jana ni watoto na wanawake, ikisemekana kuwa lengo ni kuchafua ziara ya Clinton aliekwenda na ujumbe wa kuimarisha ushirikiano kati ya Marekani na Pakistan na kuunga mkono jitahada za serikali ya Pakistan kupiga vita ugaidi katika maeneo yanayotumiwa kama maficho na wanamgambo wa Taliban na Al-Qaeda karibu na mpaka wa Afghanistan. Clinton alisema:

"Pakistan hivi sasa inapambana dhidi ya makundi katili yenye misimamo mikali yakiwa na azma ya kuwaua watu wasio na hatia na kuwatisha wananchi. Lakini nataka mjue kuwa vita hivi si vya Pakistan peke yake."

Umwagaji damu wa hiyo jana nchini Pakistan na mashambulizi yanayoshika kasi Afghanistan yamesababisha sauti kupazwa nchini Marekani. Wanasiasa wa Marekani wametoa mwito kwa Rais Barack Obama kupeleka upesi vikosi zaidi nchini Afghanistan kupambana na uasi wa Wataliban.

Hakuna aliedai kuhusika na shambulizi la hiyo jana, lakini kwa sababu ya wimbi la mashambulizi yanayotokea katika sehemu mbali mbali za Pakistan, serikali imelazimika kupeleka kiasi ya wanajeshi 30,000 katika wilaya ya Waziristan kupambana na wanamgambo wa Al-Qaeda na Taliban waliopiga kambi katika eneo hilo linalopakana na Afghanistan.

Mripuko wa hiyo jana katika soko lililojaa watu umedhihirisha kiwango cha hatari inayokabiliwa na Pakistan kutoka waasi waliopania kuleta vurugu nchini humo. Hilo ni shambulizi baya kabisa kufanywa nchini Pakistan tangu lile lililomlenga waziri mkuu wa zamani wa nchi hiyo Benazir Bhutto na kuua kama watu 140 hapo Oktoba mwaka 2007.

Clinton anaefanya ziara ya siku tatu nchini Pakistan kwa azma ya kutetea sera za Marekani zinazokosolewa amesema kuwa wanajaribu kutumia teknolojia mpya pamoja na jeshi la Pakistan kupambana na uasi katika maeneo ya mvutano. Amesema, Marekani inataka kufungua ukurasa mpya katika uhusiano wake na Pakistan. Clinton ameahidi msaada wa dola milioni 85 kupambana na umasikini na dola milioni 125 kusaidia sekta ya nishati nchini Pakistan ambako ugavi wa umeme ni tatizo kubwa.

Hii leo, Clinton ametembelea mji wa utamaduni Lahore kuzuru sehemu zenye umuhimu wa kihistoria na kidini.

Mwandishi:P.Martin/AFPE

Mhariri:M.Abdul-Rahman