Pakistan yaombwa kusitisha adhabu ya kifo
27 Desemba 2014Ban Ki Moon alizungumza na Waziri Mkuu wa Pakistan Nawaz Sharif siku ya Alhamisi kutoa salamu zake za rambi rambi baada ya shambulizi la Kaskazini Magharibi mwa mji wa Peshawar wiki iliopita katika shule moja ya kijeshi, lililosababisha mauaji ya watu 150 wakiwemo watoto 134.
Baada ya shambulizi hilo serikali ya Pakistan iliondoa marufuku ya adhabu ya kifo na tayari imeshawanyonga watu sita walio na kesi zinazohusiana na ugaidi. Pakistan inapanga kuwanyonga wanamgambo wengine 500 katika wiki kadhaa zijazo.
Waziri Mkuu Nawaz Shariff awali alitangaza kuundwa kwa mahakama ya kijeshi itakayoshughulikia kesi za Ugaidi ili kuharakisha hukumu zao.
Hata hivyo msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amesema Katibu Mkuu Ban pamoja na Waziri Mkuu Nawaz Sharif katika mazungumzo yao walitambua umuhimu wa demokrasia, utawala wa sheria na umuhimu wa kuwa na mahakama huru na kuheshimu maamuzi ya watu wa Pakistan. Waziri Mkuu wa Pakistan alimuhakikishia Ban Ki Moon kwamba kanuni zote za sheria zitaheshimiwa.
Kamanda wa Taliban auwawa na maafisa wa polisi
Huku hayo yakiarifiwa maafisa wa usalama nchini Pakistan wamesema wamemuua kamanda mmoja wa Taliban anayedaiwa kupanga mauaji yaliotokea mjini Peshawar.
Kamanda huyo aliyetambuliwa kwa jina moja tu "Saddam", anadaiwa kuuwawa siku ya Alhamisi katika ufyatulianaji risasi kati ya wanamgambo na vikosi vya usalama katika eneo la Khyber unaopakana na mji wa peshawar kulikofanyika mauaji makubwa wiki iliopita.
"Kamanda Saddam ni gaidi mkubwa aliyeuwawa katika tukio la ufyatulianaji risasi katika eneo la Jamrud mjini Khyber, washirika wake sita walijeruhiwa katika makabiliano hayo na wamekamatwa," alisema afisa mmoja wa polisi Ali Shah katika mkutano na waandishi habari.
Shah ameongeza kuwa maafisa wa serikali wanaendelea kuwahoji magaidi waliojeruhiwa, huku akimuelezea Saddam kamanda aliyekuwa muhimu kwa kundi la wanamgambo wa Taliban na aliyepanga mashambulizi kadhaa ya kigaidi.
Wanamgambo wa Taliban pamoja na wanamgambo wengine wamekuwa wakijificha mjini Khyber kutoka kwa oparesheni kaliya kijeshi dhidi yao iliozinduliwa mwezi Juni Kaskazini mwa Waziristan, eneo jingine la ukabila lililopakana na mpaka wa Afghanistan.
Eneo hilo limeendelea kuwa ngome ya magaidi wa kund la Al Qaeda na wanamgambo wa Taliban tangu mapema mwaka wa 2000.
Kwengineko maafisa wa usalama wamesema shambulizi la angani lililofanywa na ndege zisizokuwa na rubani za Marekani siku ya ijumaa dhidi ya ngome katika eneo la Taliban Kaskazini mwa Waziristan yamesababisha mauaji ya wanamgambo wanne, hili likiwa tukio la pili ndani ya wiki moja.
Shambulizi jengine katika eneo hilo lililofanyika tarehe 20 Desemba lilisababisha mauaji ya wanamgambo watano. Hata hivyo ni marufuku kwa waandishi habari kuingia katika eneo hilo hali inayokuwa ngumu kwa waandishi hao kuthibitisha idadi ya mauaji na kuwatambua waliouwawa.
Mwandishi Amina AbubakarAFP/AP
Mhariri Sekione Kitojo