1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pakistan yataka kufanyike mazungumzo kati yake na India

Zainab Aziz Mhariri: Saumu Yusuf
27 Februari 2019

Waziri Mkuu wa Pakistan Imran Khan amemtolea wito Waziri Mkuu wa India Narendra Modi wa kufanya mazungumzo kwa ajili ya kuutatua mvutano unaoongezeka kati ya nchi hizo mbili jirani zinazomiliki silaha za nyuklia.

https://p.dw.com/p/3ECmT
Indien | Indian Air Force Sukhoi Su-30MKI Jet
Picha: picture-alliance/dpa/AP Photo/S. Das

Waziri mkuu wa Pakistan Imran Khan amesisitiza kuwa vita havitalisaidia taifa lolote na kwamba ana matumaini kwamba busara itatumika. Katika hotuba yake kwenye televisheni kwa taifa, Khan alisema Pakistan iko tayari kushirikiana na India na kuongeza kuwa ni vyema viongozi hao wakaketi pamoja na kuzungumza ili kupata suluhisho.

Khan ameahidi kushirikiana na India kuwasaka na kuwatia mkononi wahalifu waliohusika na mashambulizi ya kujitoa mhanga yalioulenga msafara wa wanajeshi wa India katika sehemu ya Kashmir inayodhibitiwa na India. Wanajeshi 40 wa India waliuawa katika shambulio hilo.   

Kundi la Jaish-e-Mohammad lililopo nchini Pakistan lilidai kuhusika mashambulio hayo. Taarifa ya kundi hilo ilisema mshambuliaji wa kujitoa mhanga alitoka katika upande wa Kashmir unaodhibitiwa na India. India kwa muda mrefu imeilaumu Pakistan kwa kuwahifadhi wapiganaji wanaoipinga India madai yanayopingwa na Pakistan.

Waziri Mkuu wa India Narendra Modi
Waziri Mkuu wa India Narendra ModiPicha: Reuters/N. Chitrakar

Wakati huo huo Uturuki imeelezea wasiwasi wake juu ya kuongezeka mvutano kati ya Pakistan na India. Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Mevlut Cavusoglu amewaambia waandishi wa habari leo Jumatano kuwa India na Pakistan zinapaswa kuepuka hatua zozote ambazo zitasababisha kuongezeka zaidi mvutano kati ya nchi hizo mbili.Cavusoglu amesema ni muhimu mgogoro wa Kashmir kutatuliwa, na kuongeza kuwa Uturuki iko tayari kutoa mchango wake katika kutafuta suluhisho.

Wakati huo huo mashirika ya ndege kadhaa, ikiwa ni pamoja na Emirates na Qatar yamesimamisha safari zake za ndege kwenda Pakistan siku ya Jumatano baada ya taifa hilo la Kusini mwa Asia kufunga anga yake kufuatia mvutano kati yake na nchi jirani ya India.

Afisa mmoja wa India aliliambia shirika la habari la Reuters kwamba mashirika ya ndege yanayotumia anga za India na Pakistan kwenda bara Ulaya, Mashariki ya Kati na Asia yametatizwa na baadhi ya ndege zake kulazimika kubadili njia na kupitia Mumbai, magharibi mwa pwani ya India, kuweza kuingia kwenye eneo la kusini ili kuepuka anga ya Pakistan.

India mapema leo ilivifunga viwanja vya ndege kadhaa katika sehemu ya kaskazini ya nchi hiyo kwa muda mfupi. Hata hivyo shughuli katika viwanja hivyo vya ndege vya India zimeanza tena.

Vyanzo: /AP/RTRE