1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaPakistan

Pakistan yazizima baada ya kukamatwa kwa Imran Khan

10 Mei 2023

Hali ya wasiwasi imetanda Pakistan waziri mkuu wa zamani Imran Khan akitarajiwa kufikishwa mahakamani baadae leo na wafuasi wake wakijiandaa kwa maandamano kila kona ya nchi.

https://p.dw.com/p/4R8hz
Pakistan I Verhaftung von Imran Khan
Picha: Ahmed Khan/AFP

Pakistan inazizima, hali ya wasiwasi ikiwa imetanda kote, siku moja baada ya kukamatwa waziri mkuu wa zamani, Imran Khan. Takriban watu 1,000 wamekamatwa katika jimbo la Punjab kufikia hii leo na mtu mmoja akiuwawa katika mji wa Quetta.

Imran Khan anafikishwa mahakamani baadae hii leo kufuatia kukamatwa kwake  jana Jumanne kwa tuhuma za kuhusishwa  na rushwa. Kiongozi huyo wa upinzani aliyewahi kuwa waziri mkuu na kuondolewa kwa nguvu na bunge atafikishwa mahakamani katika kesi ambayo jaji atatakiwa kuidhinisha hatua ya kumuweka ndani mwanasiasa huyo kwa siku nyingine 14. Serikali ya Pakistan imesisitiza kukamatwa kwake hakuja chochewa kisiasa.Ahsan Iqbal ni waziri wa mipango na maendeleo amesema hivi:

" Mahakama kuu ya Islamabad ilitangaza hatua ya kukamatwa kwake chini ya mchakato sahihi wa kisheria na chini ya mamlaka ya kisheria. Kwahivyo hatua hii haikuchochewa kwa namna yoyote kisiasa.''

Pakistan I Verhaftung von Imran Khan
Picha: Asif Hassan/AFP

Kadhia hii hata hivyo hii inaiweka Pakistan katika wasiwasi mkubwa hivi sasa yakitarajiwa maandamano kila kona ya taifa hilo. Chama cha Imran Khan Tehreek-e-Insaf kimetaka maandamano yaendelee kwa amani saa chache baada ya umma ulioghadhabishwa na hatua ya ghafla ya kukakamtwa Khan, kuyatia moto makaazi ya jenerali mwandamizi wa jeshi la Pakistan katika mji wa Lahore.

Katika mkoa wa Punjab mpaka sasa takriban watu 1,000 wamekamatwa tangu hiyo jana kwa mujibu wa polisi  na maafisa 130 wa polisi na viongozi wamejeruhiwa katika vurugu zilizotokea. Mamlaka za nchi hiyo zimefunga pia huduma za mawasiliano ya simu za mkononi  pamoja na mitando yote mikubwa ya kijamii ikiwemo Twitter,Facebook na Youtube.

Hatua hiyo imechukuliwa kufuatia maagizo ya wizara ya mambo ya ndani kwa mujibu wa msemaji wa mamlaka ya mawasiliano ya Pakistan,PTA.

Na pia haijawa wazi ni kwa muda gani hatu hiyo itaendelezwa.Kadhalika katika miji mikubwa ya Pakistan mamlaka zimekwenda mbali na kufunga pia taasisi zote za elimu ikiwemo katika mji mkuu Islamabad. Kukamatwa Imran Khan imekuwa kama hatua iliyochochea upya wasiwasi na vurugu katika nchi hiyo ambayo toka hapo inakabiliwa na matatizo ya kisiasa na kiuchumi.

Pakistan I Verhaftung von Imran Khan
Picha: Ghulam Farid/AP/dpa/picture alliance

Hali ya kisiasa

Kwa kipindi kirefu Pakistan inateswa na ukosefu wa uthabiti wa kisiasa tangu alipoondolewa kwa nguvu madarakani bwana Imran Khan kupitia kura ya bunge ya kutokuwa na imanai nae. Fahamu msikilizaji kwamba waziri mkuu huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 70 alipoteza madaraka lakini bado ni kiongozi wa upinzani mwenye umaarufu mkubwa sana nchini Pakistan na akiwa ni waziri mkuu wa saba wa zamani  kukamatwa ndani ya taifa hilo.

Jana baada ya kukamatwa kwa njia ya vurugu na jeshi akiwa mahakamani,wafuasi wake hawakukaa kimya waliyashambulia makao makuu ya jeshi katika mji wa Rawalpindi  karibu na mji mkuu Islamabad ingawa walishindwa kufika kwenye jengo kuu zinakopatikana ofisi za mkuu wa majeshi Asim Munir.

Pakistan Ex-Premierminister Imran Khan
Picha: Imran Khan/Twitter/REUTERS

Waandamanaji wengine  walijaribu kufikia makaazi ya waziri mkuu mjini Lahore lakini walidhibitiwa na polisi wa kuzuia fujo.Pamoja na hayo lakini wengine walishambulia magari yaliyokuwa yamewabeba wanajeshi na hata kuwacharaza wanajeshi  kwa fimbo. Mpaka sasa lakini inaelezwa polisi na wanajeshi hawajathubutu kufyetua risasi dhidi ya waandamanaji.

Leo(Jumatano) asubuhi polisi ilisema kiasi waandamanaji 2,000 walikuwa bado wanayazingira makaazi yaliyoteketezwa kwa moto ya Luteni jenerali Salman Fayyaz Ghani,huku wakiimba nyimbo wakisema Khan ni mstari wao wa mwisho uliovukwa na jeshi na kutokana na hali ya usalama Khan atafikishwa katika korti ya muda iliyowekwa katika eneo anakozuiliwa hivi sasa kwenye eneo la ofisi za polisi mjini Islamabad.

 

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW