1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Palestina imewasilisha ombi lake

24 Septemba 2011

Kiongozi wa Palestina Mahmoud Abbas amewasilisha hapo jana ombi rasmi mbele ya Umoja wa mataifa la kutaka eneo hilo kuwa mwanachama kamili wa Umoja huo pamoja na kutambuliwa kuwa taifa kamili

https://p.dw.com/p/12fiU
Kiongozi wa Palestina Mahmoud Abbas akiwasilisha ombi rasmiPicha: dapd

Hatua hiyo imepokelewa kwa shangwe mjini Ramallah na kuzusha miito mipya ya kimataifa ya mazungumzo ya amani.

Palästinenser Israel Demonstration für UN Mitgliedschaft in Ramallah Flaggen
Shangwe zilizotanda RamallahPicha: dapd

Abbas alimkabidhi katibu mkuu wa Umoja huo wa mataifa Ban Ki Moon barua ya kuomba uwanachama huo hatua ambayo baraza la usalama la Umoja huo litaijadili siku ya Jumatatu .

Jitihada za Palestina za kutaka kutambuliwa kuwa taifa kamili kupitia Umoja wa mataifa zimeikasirisha Israeli na Marekani. Pamekuwa na jitihada za dakika za mwisho, kando kando mwa mkutano huo wa baraza kuu la Umoja wa mataifa katika kujaribu kuishawishi Palestina, irudi badala yake kwenye mazungumzo ya amani yaliokwama na Israeli.

Pande nne za kidiplomasia zinazosimamia mazungumzo ya amani ya eneo la mashariki ya kati, Umoja wa mataifa, Marekani, Urusi na Umoja wa Ulaya, zilikubaliana masaa kadhaa baada ya hotuba ya Abbas kuhusu mpango wa isareli na Palestina kuendeleza majadiliano ili kufikiwa makubaliano muafaka kwa haraka na pasi masharti ya awali. Mazungumzo hayo ya amani yamekwama kwa mwaka kuhusu sera za Israeli kuhusu ujenzi wa makaazi na masuala mengine.

Netanjahu / Ban Ki Moon / UN
katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-moon, kulia, na waziri mkuu wa Israeli Benjamin NetanyahuPicha: dapd

Waziri mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu aliyetoa hotuba yake mara baada ya Abbas katika baraza hilo kuu, alimuomba Abbas kutilia umuhimu majadiliano ya amani.

Alimuomba kiongozi huyo wa Palestina akutane naye mjiniJerusalem au Ramallah au hata pia mjini New York Marekani ambapo wote walikuwa wanahudhuria kikao hicho cha Umoja wa mataifa.

Sehemu kubwa ya hotuba ya Netanyahu ililenga wasiwasi wa nchi yake kuhusu suala la usalama, hofu ilioonekana wazi kuwa bila ya mipango ya kiusalama, Israeli ingelikabiliwa na tishio kutoka kwa wanamgambo wenye itikadi kali za dini ya kiislamu katika taifa jipya la Palestina.

Abbas / UN / Generaldebatte
Picha: dapd

Palestina baada ya kuwasilisha ombi lake imesema inaipa baraza la usalama la Umoja huo wa mataifa muda kiasi, kuzingatia ombi hilo, lakini iwapo hilo litashindwa, huenda ikaiomba baraza kuu utambulisho ambao hautoifanya Palestina kuwa mwanachama kamili wa Umoja huo lakini utakaoiruhusu kujiunga na taasisi za kimataifa.

Ombi la Abbas linaashiria ukosefu wa imani baada ya miaka 20 ya kutofanikiwa mazungumzo ya amani yaliodhaminiwa na Marekani na wasiwasi kutokana na kupanuka zaidi kwa ujenzi wa Israeli wa makaazi katika ukingo wa magharibi.

Mwandishi: Maryam Abdalla/Rtre/Dpae