Palestina yafanya mkutano wa kwanza wa serikali eneo la Gaza
3 Oktoba 2017Waziri Mkuu wa Wapalestina Rami Hamdallah ameongoza mkutano wa kwanza wa serikali katika eneo la Gaza kama sehemu ya juhudi za kutafuta maridhiano kumaliza mgogoro ambao umedumu kwa miaka 10 kati ya chama cha Fatah na kundi la Hamas.
Baada ya mkutano huo wa kwanza uliofanyika katika maakazi rasmi ya rais wa Mamlaka ya Wapalestina Mahmoud Abbas huko Gaza, Waziri Mkuu wa Wapalestina Rami Hamdallah amesema yupo tayari kuchukua usukani kuyasuluhisha masuala ambayo hayajashughulikiwa kuhusu ukanda huo wa pwani, na yanayohusu makaazi ya Ukingo wa Magharibi.
Katika maafikiano yao muhimu, kundi la Hamas limekubali kumkabidhi Hamdallah majukumu yote. Hii hapa kauli ya Al Hamdallah. "Leo tumerudi Gaza kusuluhisha vizingiti vyote, na tuufungue mlango kwa matumaini, nia na umoja na tuipatie nafasi serikali ya kitaifa iliyoafikiwa kwa pamoja kutekeleza majukumu yake yote katika sekta zote na kw aushirikiano na vyama vyote vya Palestina"
Kundi la Hamas lilidhibiti mamlaka katika ukanda wa Gaza mnamo mwaka 2007 baada ya kupambana na vikosi vya usalama vitiifu kwa Rais Mahmoud Abbas.
Ushawishi wa Misri na nchi za Kiarabu
Mchakato huo wa kusaka maridhiano ambao umeanza na vikao vya serikali ulitokana na ushawishi wa Misri pamoja na mataifa ya Kiarabu ambayo ni washirika wa Marekani. Huo ni mkutano kwanza wa baraza la mawaziri ndani ya Gaza tangu mwaka 2014, na umejiri siku moja baada ya Hamdallah kuingia katika eneo hilo tangu serikali ya pamoja ilipoanguka mnamo Juni mwaka 2015.
Mwezi uliopita, kundi la Hamas linalotazamwa na Israel na nchi za Magharibi kama kundi la kigaidi, liliivunja serikali yake ya kivuli baada ya Misri, Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu kuiwekea Qatar vikwazo vya kiuchumi ambayo ndiyo mdhamini wake mkuu.
Tashwishi kuhusu maafikiano mapana
Zaidi ya watu milioni mbili wanaishi katika eneo hilo maskini la Gaza, na ambalo limewekewa vizuizi na Israel na Misri kwa miaka mingi.
Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa katika Mashariki ya Kati Nickolay Mladenov amesema ana matumaini kuhusu mazungumzo hayo ya Amani lakini kwa tahadhari.
Hata hivyo wachambuzi bado wana wasiwasi kuhusu uwezekano wa maafikiano mapana kati ya pande hizo mbili.
Mwandishi: John Juma/AFPE/RTRE/APE
Mhariri: Yusuf Saumu