Palestina yazika wahanga, yailaani Marekani
16 Desemba 2017Afisa wa ngazi za juu kwenye serikali ya Palestina, Nabil Abu Rudeineh, ameliambia shirika la habari la WAFA kwamba kamwe Wapalestina hawatakubali mabadiliko yoyote kwenye mpaka wa 1967 wa Jerusalem Mashariki.
"Msimamo huu wa Marekani unathibitisha kwa mara nyengine kwamba utawala wa sasa wa nchi hiyo haupo kabisa kwenye suala la kupatikana amani na badala yake unataka kuuimarisha ukaliaji wa kimabavu," alisema.
Afisa mmoja wa ngazi za juu wa Marekani alisema kabla ya kuanza kwa ziara ya Makamu wa Rais Mike Pence kwenye mataifa ya Misri, Israel na Ujerumani, kwamba nchi hiyo haiwezi kuona "ni kwa namna gani Ukuta wa Magharibi usiwe sehemu ya Israel" hata ikiwa patakuwa na makubaliano baina ya Waisraeli na Wapalestina.
Ukuta huu, ambao ni mabaki ya upande wa magharibi wa Hekalu la Pili, ni sehemu takatifu kwa Mayahudi wengi na ni sehemu ya eneo pana lililogeuka kiini cha mzozo wa kidini kwenye mji wa Jerusalem, likifahamika kama Mlima wa Hekalu kwa Mayahudi na Makaburi Matakatifu kwa Waislamu.
'Mashahidi' wazikwa
Haya yanatokea katika wakati ambapo Wapalestina wakiwazika wahanga wa hivi karibuni kabisa wa mashambulizi ya Israel dhidi ya waandamanaji wanaopinga tamko la Rais Donald Trump wa Marekani la kuitambua Jerusalem kuwa mji mkuu wa taifa hilo la Kiyahudi.
Miongoni mwa watu wanne waliouawa jana (Ijumaa) na kuzikwa leo, ni kijana wa Kipalestina aliyekuwa amekatwa miguu katika mashambulizi ya Israel ya miaka tisa iliyopita.
Ibrahim Abu Thuraya, aliyekuwa na miaka 29, aliuawa akiwa kwenye kigari chake cha magurudumu mawili jana kwenye Ukanda wa Gaza. Afisa mmoja wa jeshi la Israel alisema kuwa matukio kuhusika na mauaji ya Abu Thuraya yalikuwa yakichunguzwa, huku maafisa wa afya wa Palestina wakisema kijana huyo hakuwa kitisho chochote kwa jeshi la Israel.
Kwa wiki ya pili mfululizo, maeneo ya Ukingo wa Magharibi na Ukanda wa Gaza yamekumbwa na maandamano na machafuko, kufuatia tangazo la Trump na pia hatua ya kuagiza kuhamishwa kwa ubalozi wa nchi yake mjini Tel Aviv kwenda Jerusalem. Takribani ulimwengu mzima umelaani hatua hii, kasoro Marekani na Israel yenyewe.
Mataifa ya Kiislamu yaja juu
Katika kile kinachoonekana kama kulipiza kisasi, mataifa ya Kiislamu nayo yalitangaza kuitambua Jerusalem Mashariki kuwa mji mkuu wa Palestina kwenye mkutano wa dharura ulioitishwa na Uturuki wiki hii.
Vile vile, kuna mipango ya kuifanya Palestina itambuliwe kama mwanachama kamili wa Umoja wa Mataifa, na huku Uturuki ikitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuulaani uamuzi wa Trump.
Vuguvugu la kijeshi la Hamas, ambalo linatawala Ukanda wa Gaza, limekuwa na msimamo mkali zaidi, likisema kwamba Jerusalem "ni mji wa Kiislamu na Kiarabu" na ikikataa muafaka wowote juu ya hilo.
Mwandishi: Mohammed Khelef/dpa
Mhariri: Caro Robi