Pambano la der Klassiker Bayern na BVB lapoteza ladha yake
11 Novemba 2019Ligi ya Ujerumani Bundesliga imeendelea wiki hii ikitimiza mchezo wake wa 11, ambapo hadi sasa vinara ni Borussia Moenchengladbach, ambayo hapo jana jioni iliizaba Werder Bremen kwa mabao 3-1 na kufungua mwanya wa pointi 4 wakiwa na pointi 25 wakiitangulia RB Leipzig inayoshika nafasi ya pili ikiwa na pointi 21.
Mlinda mlango wa Gladbach Yann Sommer anasifu mafanikio ya timu yake hadi sasa.
"Bila shaka inapendeza, wakati juhudi zetu zimefanikiwa na kwa kuwa tumeonesha juhudi katika uwanja wetu wa nyumbani wa Borrusia Park. Tunawekeza nguvu nyingi sana,katika mchezo. Tuna uwezo mkubwa wa kumalizia. Nafikiri , kwa hivi sasa pia kuwa ndio ufunguo wa mafanikio. Tunahitaji magoli, kwa kuwa tunacheza mpira, ambao una kaa katika miguu yetu. Na iwapo katika hali hii tunapata mafanikio, tunaweza kila mara kupumzika wakati mchezo ukiendelea. Kwa hivi sasa kila kitu kinakwenda vizuri."
Mabingwa watetezi Bayern Munich wanashika nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi, baada ya kuirarua Borussia Dortmund siku ya Jumamosi kwa mabao 4-0. Mchezo ambao unaangaliwa hapa Ujerumani kama mchezo wa mafahali wawili der Klassiker ulimalizika, kwa aina ya mpambano wa kati ya mbuzi na ng'ombe kwani Borussia Dortmund kwa mara ya tano sasa wanachezea kichapo cha hali ya juu katika uwanja wa Allianz Arena nyumbani kwa Bayern. Nini tatizo la Borussia Dortmund wakutanapo na Bayern katika uwanja wa Allianz Arena: Swali hiyo analijibu mshambuliaji wa Bayern Munich Thomas Mueller.
„Ndivyo walivyo, kwa kweli wakati BVB wanakutana na timu yetu, wana watu wengi wataalamu, ambao kimbinu ni wazuri sana, lakini nafikiri , mchanganyiko huo unaleta tu sura ya kimwili na unadhifu. Ni lazima uwe na kikosi chenye mshikamano katika uwanja na leo mtu anaweza kusema, tulikuwa na kikosi kilichochangamka na kufanya juhudi tukiwa na mpira, lakini pia bila mpira na hatukuwapa Dortmund nafasi ya kupumua."
Hayo ndio masaibu yaliyowakuta Borussia Dortmund mjini Munich mwishoni mwa juma, ambapo wangependa kusahau haraka. Dortmund iko hivi sasa katika nafasi ya 6 ikiwa na pointi 19 na mchezo wao na bayern haukuwapendeza mashabiki na pia viongozi wa timu hiyo. Huyu hapa mkurugenzi wa spoti wa Borussia Dortmund Michael Zorc:
„Tumefanya makosa mengi kirahisi katika mchezo wetu wa kumiliki mpira, tumewarahisishia sana Bayern. Na hatukuwamo katika mchezo kabisa. Mwishowe waweza kusema, hatukuonesha juhudi. Hakukuwapo na juhudi yoyote katika mchezo wetu hii leo."
timu iliyofaidika sana na mchezo huu wa 11 katika Bundesliga ni pamoja na SC Freiburg ambayo iliiangusha Eintracht Frankfurt nyumbani kwa bao 1-0 na kujikingia pointi 21 katika michezo 11 hatua ambayo ni mafanikio makubwa ya kwanza ya Freiburg katika muda wa miaka zaidi ya 20. Freiburg imepanda hadi nafasi ya 4 ya msimamo wa ligi na huyu hapa ni kocha wa timu hiyo Christian Streich:
"Huwezi kuamini , tumefurahi kiasi gani. Tuna pointi 21 baada ya michezo 11. Kwetu sisi hilo ni jambo la ajabu, na hivyo ndivyo ilivyo, kwamba , pointi hizo hatukuiba. Tuna timu yenye kujielewa. Leo tulikuwa sawa. Pengine Frankfurt walipata nafasi bora zaidi za kupata mabao, lakini sisi ndio tulifunga goli. Ndivyo ilivyo ilishawahi kutokea."
Wakati huo huo nahodha wa Eintracht Frankfurt David Abraham anakabiliwa na adhabu kali kutoka katika shirikisho la kandanda la Ujerumani DFB baada ya kumwangusha chini kocha wa Freburg Christian Streich katika pambano lao la jana Jumapili la Bundesliga. Abraham alioneshwa kadi nyekundu na mwamuzi kwa tukio hilo katika dakika za mwisho za mchezo huo ambao Freiburg ilishinda kwa bao 1-0. Abraham anaweza kukabiliwa na kukaa nje ya uwanja kwa muda mrefu.