1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pande hasimu zalaumiana juu ya kukiukwa makubaliano, Yemen

Zainab Aziz Mhariri:Yusuf Saumu
5 Aprili 2022

Pande zinazozozana nchini Yemen leo zimelaumiana juu ya kukiukwa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano, ikiwa ni siku tatu tu baada ya kufikiwa makubaliano hayo yaliyoanza kutekelezwa mwanzoni mwa mwezi wa Ramadhani.

https://p.dw.com/p/49Uck
Jemen | Luftangriff auf Sanaa
Picha: Khaled Abdullah/REUTERS

Serikali inayotambuliwa kimataifa, inayoungwa mkono na muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia, na waasi wa Kihouthi wanaoungwa mkono na Iran wamekuwa katika mvutano wa kuwania madaraka tangu mwaka 2014, wakati waasi hao walipouteka mji mkuu Sanaa. Mapatano hayo ya miezi miwili yalitoa mwanga wa matumaini katika mzozo huo unaozingatiwa kuwa mzozo mbaya zaidi wa kibinadamu duniani.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Yemen, Ahmed bin Mubarak, amewalaumu Wahouthi kwa kukiuka makubaliano hayo ya kusitisha mapigano. Waasi wa Houthi hawakujibu moja kwa moja madai hayo, lakini vyombo vyao vya habari vimeripoti juu ya ukiukwaji makubaliano ya kusitisha mapigano ambayo yanafanywa na wanajeshi wanaoiunga mkono serikali.

Waasi wa Houthi wa nchini Yemen
Waasi wa Houthi wa nchini YemenPicha: Mohammed Hamoud/NurPhoto/picture alliance

Mjumbe maalum wa Marekani kwa Yemen, Tim Lenderking, ameiambia televisheni ya Bloomberg leo Jumatatu kwenye mahojiano kwamba pande zote kwenye mzozo huo zilionyesha utayari wa kutoa ushirikiano pamoja na kwamba hakuna upande uliopata yote wanayoyataka. Amesema huu ni wakati muhimu sana kwa Yemen, katika hatua inayoweza kuwapa Wayemen ahueni baada ya nchi hiyo kukabiliwa na mzozo kwa muda wa miaka saba.

Chini ya makubaliano ya hivi punde ya kusitisha mapigano yaliyosimamiwa na Umoja wa Mataifa, operesheni zote za kijeshi za ardhini, angani na majini, zikijumuisha na mashambulizi yanayovuka mpaka, zinakusudiwa kusimamishwa. Meli 18 za mafuta zitaruhusiwa kuingia katika bandari ya Hodeida na safari mbili za ndege za kibiashara kwa wiki pia zitaruhusiwa kuingia na kutoka katika uwanja wa ndege wa Sanaa unaodhibitiwa na wahouthi.

Mwanamfalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman.
Mwanamfalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman.Picha: SAUDI PRESS AGENCY/VIA REUTERS

Taarifa za kusitisha mapigano zilitolewa wakati mazungumzo juu ya mzozo wa Yemen yalikuwa yakifanyika nchini Saudi Arabia lakini bila ya wahouthi, ambao wamekataa kuhudhuria mazungumzo hayo kwa kile wanachosema yanafanyika katia ardhi ya adui yao. Rais wa Yemen Abedrabbo Mansour Hadi, katika hotuba yake ya leo Jumatatu katika mji mkuu wa Saudi Arabia, Riyadh, amewataka Wahouthi kurejea kwenye meza ya mazungumzo ili kuinusuru nchi iliyogawika.

Wayemeni wana matumaini makubwa licha ya makubaliano kadhaa ya kusitisha vita ya hapo awali hayaukufaulu. Vita vya wenyewe kwa wenyewe vimesababisha vifo vya maelfu ya watu huku takwimu za Umoja wa Mataifa zikiashiria jinsi vita hivyo vilivyoitumbukiza Yemen kwenye baa la njaa.

Chanzo: AFP